Serikali yaombwa iruhusu usafirishaji mabuu ya vipepeo

SERIKALI imeombwa iruhusu usafirishaji wa mabuu ya vipepeo nje ya nchi, ili kuwasaidia wafugaji wa vipepeo kuendelea kujipatia kipato.

Rai hiyo imetolewa leo Septemba 17,2022 mjini Morogoro na wadau wa mazingira na uhifadhi katika kikao cha uwasilishaji wa rasimu ya mkakati wa masoko ya mazao yanayozalishwa katika miradi ya jamii inayofadhiliwa  na Mfuko wa  Uhifadhi wa Milima ya  Tao la Mashariki (EAMCEF).

Wafugaji zaidi ya 360 kutoka kwenye vijiji vinavyopakana na milima ya Amani na Usambara, iliyopo katika safu ya milima ya Tao la Mashariki walikuwa wakijishughulisha na ufugaji wa vipepeo na usafirishaji mabuu ya vipepeo nje ya nchi tangu mwaka 2004 na hadi serikali, ilipositisha mwaka  2016.

Mtafiti Mkuu wa  Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI), Dk Pilly Kagosi alisema kuwa, biashara ya usafirishaji wa mabuu ya  vipepeo ilikuwa inawapatia kipato wananchi na hivyo kuondokana na uhafribifu wa misitu ya Milima ya Tao la Mashariki,  hususani milima ya Amani na Usambara.

“ Kaya zaidi ya 300 zilikuwa zinajishughulisha na biashara hii na sasa hawafanyi tena, baada ya serikali kuzuia usafirishaji wa viumbe hai,” alisema Dk Kagosi.

Dk Kagosi alisema hivi sasa  kuna hatari kwa kaya zilikuwa zinatengemea biashara ya ufugaji wa vipepeo na usafirishaji wa mabuu ya vipepeo nje ya nchi kurudi tena kuharibu misitu, ili kujipatia kipato.

“Hizi jamii sasa zimekata tamaa na baadhi wameanza kurudi tena kufanya na uharibifu wa misitu kwenye safu ya milima ya Tao la Mashariki, “  alisema Dk Kagosi.

Hivyo aliiomba serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, kuangalia namna ya kipekee  na nzuri ya kusaidia kuendelea kwa biashara ya usafirishaji mabuu ya vipepeo nje ya nchi, kwani kutasaidia kulinda uharibifu wa misitu ya jamii.

Dk Kagosi pia alisema, ni vyema maeneo ya uzalishaji na ufugaji wa vipepeo yakawekewa mazingira mazuri ya miundombinu, wezeshi ya utalii kwa ajili ya kuwavutia wageni, wakati serikali ikiangalia namna bora ya kuruhusu usafirishaji nje ya nchi.

Naye mwalimu wa ufugaji vipepeo, James Msuya alisema, kupitia ufugaji na usafirishaji wa mabuu ya vipepeo nje ya nchi, wananchi walikuwa na uwezo wa kujipatia kipato cha Sh 300,000 kwa mwezi na wale wenye juhudi kubwa walifikisha Sh 600,000  hadi Sh 800,000 kwa mwezi.

Msuya ambaye pia ni mtafiti na mfanyakazi wa zamani wa Shirika la Kuhifadhi Mazingira  Asili  mkoani Kilimanjaro, alisema, mradi wa ufugaji wa vipepeo uliwasaidia wananchi wanaoishi karibu na misitu ya Amani, Usambara na Shengena, iliyopo  kwenye mikoa ya Kilimanjaro na Tanga,  ambayo inaunda safu ya  Milima ya Tao la Mashariki  kushiriki kwenye uhifadhi wa misitu.

“ Uhifadhi wa milima ya Tao  la mashariki  hasa eneo la Amani , Usambara na Shengena ipo hatarini  kwa uharibifu wa mazingira tangu  baada ya serikali kusitisha usafirishaji wa mabuu ya  vipepeo  katika kukuza  uchumi wao, “ alisema Msuya

Habari Zifananazo

Back to top button