Serikali yaongeza kasi madaraja kukuza uchumi   (Kimkakati)

Serikali yaongeza kasi madaraja kukuza uchumi  

SERIKALI imejizatiti kuendeleza na kukamilisha ujenzi wa madaraja nchini yakiwemo ya kimkakati katika mwaka huu wa fedha 2022/23.

Ujenzi wa miradi hiyo ya madaraja ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26).

Ilani hiyo katika ukurasa wake wa 67 na 68 inabainisha miradi ya madaraja iliyokamilika kujengwa na ile inayoendelea kujengwa wakati Mpango wa Maendeleo (Uk 31) ukieleza kuhusu kukamilika kwa ujenzi wa madaraja makubwa 12 likiwemo Daraja la Magufuli Mto Kilombero.

Advertisement

Mpango huo wa Maendeleo pia unatambua kuendelea kwa shughuli za ujenzi wa madaraja mengine likiwemo Daraja la Kigongo–Busisi, Sukuma, Simiyu, Mkenda, Mtera, Godegode, Malagarasi Chini na Ugalla. Pia lipo Daraja la J.P. Magufuli la Kigongo-Busisi mkoani Mwanza.

Kukamilika kwa miradi hiyo kutafungua uchumi wa wananchi na uchumi wa nchi kwa kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na watu.

Hivi karibuni Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alivieleza vyombo vya habari Dar es Salaam kuwa daraja la Kigongo-Busisi lenye urefu wa kilometa 3.2 na barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 1.66, ujenzi wake unaendelea vizuri.

Wakati akiwasilisha bungeni mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya wizara hiyo kwa mwaka huu wa fedha, Profesa Mbarawa alisema hadi Aprili mwaka huu ujenzi wa mradi huo ulikuwa umefikia asilimia 40.18.

“Katika mwaka wa fedha 2022/23, jumla ya shilingi milioni 7,000.00 zimetengwa kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa daraja hili na barabara unganishi,” aliwaeleza wabunge.

Daraja lingine ambalo ujenzi wake unaendelea katika kipindi cha mwaka huu ni Daraja la Mzinga katika Barabara ya Mbagala Rangi Tatu–Kongowe mkoani Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa wizara hiyo, daraja hilo limetengewa Sh milioni 500.00 kwa ajili ya kuendelea na maandalizi ya ujenzi wake.

Kuhusu ujenzi wa Daraja jipya la Wami lenye urefu wa mita 513.5 katika barabara ya Chalinze-Segera mkoani Pwani, alisema limetengewa Sh milioni 2,000.00 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi katika mwaka huu wa fedha.

Profesa Mbarawa alisema bungeni kuwa ujenzi wa daraja hilo ulikuwa umefikia asilimia 72.88 wakati Daraja la Ugalla mkoani Katavi limetengewa Sh milioni 500.00 kwa ajili ya kuendelea na maandalizi ya ujenzi.

“Aidha, hadi Aprili mwaka huu, ujenzi wa Daraja la Kitengule na barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 18 umekamilika na kazi ya ujenzi wa barabara unganishi inaendelea na kwa ujumla mradi umefikia asilimia 73.89,” alisema Profesa Mbarawa akiwa bungeni.

Profesa Mbarawa alizitaja kazi nyingine zinazoendelea kuwa ni pamoja na ujenzi wa Daraja la Msingi mkoani Singida ambalo limefikia asilimia 81 na ununuzi wa madaraja ya chuma ambao uko katika hatua za mwisho.

Alisema kazi nyingine zinazoendelea ni usanifu wa kina wa Daraja la Malagarasi Chini mkoani Kigoma huku taratibu za manunuzi ya kumpata mkandarasi wa ujenzi wa barabara unganishi katika Daraja la Sibiti mkoani Singida nazo zinaendelea.

 

 

 

 

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *