WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni ameonya taasisi, mashirika na viongozi wa dini wanaotumia dini kuhamasisha mambo yanayovunja maadili, mila na desturi za Kitanzania.
Pia, amezitaka taasisi na mashirika ya dini kutafuta suluhu ya migogoro kwa kupitia upya katiba za taasisi hizo badala ya kutumia muda na rasilimali kushughulika na utatuzi wa migogoro badala ya kuwahudumia waumini.
Masauni alisema hayo Dar es Salaam jana katika kikao na viongozi wa mashirikisho na mabaraza ya kidini, kilicholenga kujadili masuala mbalimbali ikiwamo kuboresha ushirikiano baina ya serikali na taasisi za dini nchini.
Alisema kumekuwa na changamoto ya uanzishwaji wa taasisi za kidini pasipo kufuata sheria na akasema Sheria ya Jumuiya Sura ya 337 inataka kila kikundi au Jumuiya kusajiliwa ili iweze kufanya shughuli zake.
“Lakini wote sasa ni mashuhuda kuwa zipo taasisi nyingi katika jamii yetu ambazo zinajiendesha pasipo kusajiliwa na hata uendeshwaji wake ni wa kutia mashaka.
Nitoe wito kwenu kuwa tusaidiane katika kutoa elimu na kwa jamii kuhusu umuhimu wa kusajili Jumuiya na vikundi,” alisema.
Alisema pale itakapoonekana kuna jumuiya au vikundi vya kidini ambavyo uendeshwaji wake ni wa kutia shaka ni vema wananchi wakashirikiana na Ofisi ya Msajili katika kuzibaini jumuiya za namna hiyo ili kuiweka jamii katika hali ya usalama na amani.
Akijibu swali kuhusu kiongozi wa dini anayejiita Zumaridi anayefanya mahubiri yake huku akijiita Mungu, alikiri kuwa huyo ni mmojawapo wa taasisi za dini zinazofanya shughuli zake bila kusajiliwa.
“Kuna taasisi zimekuwa zikiibuka bila hata kusajiliwa akiwamo huyo unayemtaja, hakujasajiliwa. Ni mtu ametoka huko anasema yeye ni kiongozi wa dini, wapo wengine unakuta anahamasisha mambo ya jinsia moja mwingine anasema yeye ni Mungu mwingine anazungumza vitu vya ajabu,” alisema Masauni.
Alisema vitendo hivyo ni kinyume na sheria, maadili ya nchi na mila na desturi za Kitanzania. “Kwa hiyo, tutaendelea kupambana nalo, ni kama vile Jeshi la Polisi lipo mtu akiiba atakamatwa, hivyo viongozi au taasisi ya dini wanaotumia dini kinyume na maadili watachukuliwa hatua,” alieleza.
Alisema kwa mujibu wa sheria, taasisi za dini zinazosajiliwa zinapata udhamini kutoka kwa taasisi mama au baba zilizopo, hivyo taasisi mpya haziwezi kudhaminiwa bila taasisi hizo na kueleza kuwa ni wajibu wa taasisi zinazotoa dhamana kujiridhisha.