Serikali yaonya uuzaji mahindi yaliyopo shambani
SERIKALI imeifunga breki kampuni ya SHAFA Agro Ltd inayotuhumiwa kuwaweka baadhi ya wakulima katika hatari ya kukumbwa na baa la njaa katika kaya zao, kama wataendelea kuiuzia mahindi mabichi yaliyoko mashambani mwao.
Kampuni hiyo inayojihusisha na ufugaji wa ng’ombe, uuzaji wa maziwa pamoja na kutengeneza chakula kwa ajili ya mifugo ipo katika Kijiji cha Kidamali Kata ya Nzihi wilayani Iringa.
Akizungumzia na wanahabari Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Verronica Kessy alisema kampuni hiyo pamoja na kulima imekuwa ikinunua kutoka kwa wakulima mahindi mabichi kwa ajili ya chakula cha mifugo yake.
“Kutokana na kufunguka kwa fursa hii baadhi ya wakulima wamekuwa wakiuza mahindi yao pasipo kujali hali ya baadae ya usalama wa chakula katika familia zao,” Mkuu wa Wilaya alisema.
Alisema serikali kwa kutambua umuhimu wa usalama wa chakula inaendelea kulifuatilia kwa makini suala hilo na kwa kupitia halmashauri zake za manispaa, wilaya na vijiji inaendelea kutoa elimu na ushauri kwa wananchi unaolenga kuzingatia usalama wa chakula katika familia.
Ili kuondokana na hatari ya ukosefu wa chakula katika kaya alisema serikali inaendelea kuwashauri wananchi kuuza ziada ya chakula baada ya mavuno na watendaji wa vijiji wameagizwa kudhibiti biashara hiyo.
Kessy alisema utaratibu wa kuuza mazao baada ya mavuno utawawezesha wakulima kujua mahitaji ya familia, ziada waliyopata na kipato chao cha mwaka husika.
“Aidha tunawashauri wakulima kuanzisha mashamba maalumu ya kulima mahindi kwa ajili ya biashara hiyo huku wakiendelea na mashamba kwa ajili ya chakula,” alisema.
Alisema kwa kufanya hivyo kampuni hiyo na wakulima hao watasaidia kuuepusha mkoa wa Iringa kwa ujumla wake ba baa la njaa.
Mbali na ufugaji na uuzaji wa maziwa, kampuni hiyo kwa kupitia kiwanda chake cha Shafa Mills inazalisha pia lishe bora ya mifugo.