Serikali yapewa ushauri kuokoa fedha magerezani

WATAALAMU wa sheria wameishauri serikali irekebishe sheria ya haki jinai ikiwemo ya upelelezi ili kudhibiti wahamiaji haramu wasiingie nchini na kuwabana watu wanaowasaidia kuingia nchini.

Hivi karibuni Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, iliwaeleza wabunge kuwa serikali inatumia Sh milioni 15.54 kwa siku na Sh bilioni 5.673 kwa mwaka kuwahudumia wahamiaji haramu.

“Kiasi hicho cha fedha kinachotumika kuwatunza wafungwa/mahabusu hao kingeweza kununua madawati 81,030 kwa kila dawati kugharimu shilingi 70,000.00, kwa msingi huo kuna haja ya serikali kuepuka kutumia gharama kuwatunza wafungwa/mahabusu
haramu na kuzielekeza kwenye miradi ya maendeleo”alisema Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Vita Kawawa jijini Dodoma.

Advertisement

Vita aliwaeleza wabunge kuwa taarifa ya wizara ilionesha kuwa kwa kipindi cha Septemba hadi Desemba mwaka jana wahamiaji haramu 7,493 walikamatwa nchini.

Alisema uchambuzi uliofanywa na kamati ulibaini kuwa katika kipindi cha Septemba hadi Desemba mwaka jana katika magereza nchini kulikuwa na wafungwa na mahabusu wahamiaji haramu 3,108.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga alisema ni muhimu kurekebisha sheria ya haki jinai inayohusu upelelezi ili kuipunguzia serikali mzigo wa kuwahudumia wahamiaji haramu na mahabusu wengine.

“Kwa sababu upelelezi hauna mwisho na mtu anaweza akapeleleza hata miaka minne bila kukamilika, hiyo changamoto kubwa, ndiyo maana kwenye Tume ya Rais ya Marekebisho ya Kijinai tumepeleka pendekezo hilo kwamba sheria irekebishwe ili upelelezi ufanyike kwa haraka,”alisema Anna.

Wakili Antipas Lakam alisema moja ya sababu ya wahamiaji haramu kujaa magerezani ni ukosefu wa fedha kwa kuwa wanaweza kukiri kosa la kuingia nchini isivyo halali na mahakama ikaamuru walipe faini au kifungo.

“Wengi wao hawana hela, wanakubali kufungwa, sasa hapo ndipo kazi inaanza kwa serikali kuwahudumia wafungwa hao, na isipofanya jitihada za kuwarudisha  katika nchi zao, wataendela kuishi magerezani na kuhudumiwa na serikali,”alisema Lakam na kuongeza;

“Tatizo linakuja, mhamiaji haramu anakiri kosa ni kweli kaingia nchini isivyo halali, akiambiwa arudi kwao hana hela, je unawarudishaje watu hao? Kwa ndege? Je bajeti unayo? Hayo ni maswali mengi ambayo sio rahisi kuyatekeleza,”.

Lakam alisema jambo la msingi kwa sasa ni kudhibiti mipaka na kuzungumza na Watanzania waelewe athari za kushirikiana na wahamiaji haramu.

Alisema wahamiaji haramu wanabebwa na magari ya Watanzania, wanahifadhiwa kwenye nyumba za Watanzania hivyo mabadiliko lazima yaanzie kwenye mitazamo ya wananchi nchini.

Lakam alisema kuwarisha wahamiaji haramu ni gharama kubwa hivyo akashauri wapewe vifungo vya muda mfupi wakati serikali inawasiliana na mamlaka ya nchi zao kuhusu namna ya kuwarudisha kwao.

“Hata ukiweka adhabu kubwa haitasaidia kwa sababu hawana njia ya kuepuka matatizo yanayowakabili, kikubwa ni kuimarisha mipaka yetu na kuwasaidia wakiwa kwenye nchi zao, pia watumishi wa umma maeneo ya mikapani wawe waadilifu,

Wakili wa kujitegemea, Daniel Kalasha alisema ni vyema serikali itoe elimu ili wananchi wawe wanatoa taarifa wanapokutana na mtu wasiyemwelewa.

“Kwa mfano unaishi na mtu au wamekuja wageni hujui wametoka wapi, inatakiwa wananchi wapewe hamasa ya kutoa taarifa katika mamlaka husika ili mamlaka hizo zitimize wajibu. Mtu anamkaribisha mgeni halafu mgeni huyo anafanya jinai, hatimaye raia anapata matatizo makubwa,”alisema Kalasha.

Alisema kuna haja kwa serikali kuongeza nguvu kazi kwenye Jeshi la Uhamiaji ili kusimamia mipaka yote kwa ukamilifu na kudhibiti wimbi la wahamiaji haramu.

Kalasha alisema serikali inapaswa kuongeza nguvu kazi katika mipaka na maeneo yenye shughuli nyingi zinazoruhusu watu kuingiliana kirahisi kama vile mkoani Kagera katika eneo Mutukula, Kyaka na Kyaka-Mutukula.

*Imeandikwa na Matern Kayera na Ikunda Erick.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *