Serikali yapiga jeki utendaji Newala

MTWARA: SERIKALI imekabidhi vitendea kazi mbalimbali katika Halmashauri ya Wilaya ya Newala mkoani Mtwara ili kurahisisha utendaji kazi kwa watumishi wa halmashauri hiyo.

Akikabidhi vitendea kazi hivyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mkuu wa Wilaya ya Newala, Rajabu Kundya amesema  vifaa hivyo vitafanya kazi ya usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli mbalimbali katika sekta hizo.

Vifaa  hivyo vilivyokabidhiwa  ni   pikipiki 12 za maofisa ugani, magari mawili ya sekta ya afya pamoja na elimu (sekondari) wilayani humo huku akiishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuwaletea vifaa ambavyo sasa vinaenda kurahisisha zaidi utendaji kazi wao.

Aidha, ni muda mrefu sasa sekta hizo zilikuwa zinakabiliwa na changamoto ya usafiri hivyo upatikanaji wa vifaa hivyo utarahisisha utendaji wa kazi na kuwaletea wananchi maendeleo.

‘’Ni matarajio yetu, magari haya yatakwenda kuchochea utekelezaji wa mipango ya afya na elimu na tunatarajia tutaona mabadiliko yake maana kama tulipokuwa hatuna nyenzo hizi tulifikia kiwango kikubwa kimaendeleo basi tunatarajia kwa kupata nyenzo hizi tutapiga hatua kubwa zaidi’’amesema Kundya

‘’Tunatarajia pikipiki zitatumiwa na wenzetu wa kilimo kuhakikisha kwamba wanawafikia kwa uharaka wakulima kuwapa mbinu za kilimo bora ili tupate mafanikio makubwa zaidi katika uzalishaji’’

Aidha amesisitiza suala la mshikamano baina ya watendaji wa halmashauri hiyo, wananchi na mkoa kwa ujumla ili kuendelea kuleta maendeleo chanya kwa taifa lao.

Hata hivyo amewataka watendaji hao kufanya kazi kwa bidii ili waweze kupiga hatua zaidi kimaendeleo.

Habari Zifananazo

Back to top button