SERIKALI imepiga marufuku operesheni zote zinazofanyika kwa kuviziana na kutaka wananchi washirikishwe katika hatua zote ikiwa ni pamoja na kupewa taarifa.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa agizo hilo leo Bungeni Jijini Dodoma wakati akitoa taarifa maalum ya serikali nakutaka Mamlaka kuimarisha mipaka ya hifadhi kwa kuwekwa nguzo (beacons) ndefu zinazoonekana pamoja na mabango kama ilivyofanyika katika Hifadhi ya Ruaha, Loliondo na Isawima.
Taarifa ya Waziri Mkuu inafuatia uwepo wa ongezeko la shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo, ufugaji na makazi katika maeneo ya hifadhi kwa kujua ama kwa kutojua.
Hata hivyo, kuimarika kwa shughuli za uhifadhi kumewezesha baadhi ya Wanyama kama vile Tembo kuongezeka na hivyo kusababisha uharibifu wa mazao na wakati mwingine ulemavu na hata vifo kwa baadhi ya wananchi wanaoishi katika maeneo yanayopakana na hifadhi.
“Ongezeko la shughuli za kibinadamu ikiwemo usafishaji wa mashamba kwa ajili ya kilimo, ufugaji, uchomaji moto holela na matumizi mengine yasiyo endelevu ya rasilimali za misitu yakichagizwa na ongezeko la idadi ya watu ni miongoni mwa changamoto kubwa za uhifadhi,” Waziri Mkuu amesema bungeni.
“Athari za vitendo hivyo, tumezishuhudia kwenye baadhi ya maeneo nchini ikiwemo uharibifu katika hifadhi ya Ruaha na Bonde la mto Ruvu.”
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu hali hiyo inachangia kuleta mabadiliko ya tabianchi na athari zake kama vile ukame, kuongezeka kwa joto, mafuriko na mabadiliko ya misimu ya mvua.
Taarifa za Serikali zinaonesha kuwa kiwango cha kutoweka kwa misitu kwa mwaka kimeongezeka kutoka hekta 372,800 kwa makadirio ya mwaka 2015 hadi hekta 469,420 kwa makadirio ya mwaka 2022.
Serikali inasimamia maeneo yaliyohifadhiwa kisheria yenye ukubwa wa kilometa za mraba takriban 307,800 sawa na asilimia 32.
5 ya eneo lote la nchi. Maeneo hayo yanajumuisha hifadhi za Taifa 22, eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, mapori ya akiba 29, mapori tengefu 23, maeneo ya Jumuiya ya Hifadhi za wanyamapori 38, maeneo matatu ya ardhi oevu chini ya Mkataba wa Ramsar Site, hifadhi za misitu ya asili 465, Hifadhi za Misitu ya Mazingira asilia 20, Mashamba ya Miti ya Serikali 24, hifadhi za nyuki 10, maeneo ya malikale 133 na vituo saba vya Makumbusho ya Taifa.
Waziri Mkuu ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii ifanye ufuatiliaji wa malalamiko ya wananchi kuhusu tabia ya baadhi ya Wahifadhi kuswaga mifugo na kiingiza hifadhini kwa lengo la kuitafisha na kujipatia fedha. Aidha ichukue hatua kali kwa Watumishi watakaobainika kufanya vitendo hivyo.
Vilevile ametaka wahifadhi kuimarisha mahusiano ya ujirani mwema na kutoa elimu kwa wananchi wanaopakana na hifadhi kuhusu manufaa ya uhifadhi endelevu.