Serikali yapigilia msumari utunzaji mazingira nchini

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango ametoa mwito kwa Watanzania walione suala la kutunza mazingira kama ni vita.
Dk Mpango ameomba viongozi wa dini zote na madhehebu yote kuwasisitiza waumini wao waone suala la usalama wa mazingira ni jambo muhimu.
“Na tumeagizwa kwenye maandiko matakatifu, Mungu alitupa bustani nzuri hii tuitunze, ”alisema.
Dk Mpango alisema hayo jana baada ya yeye na mkewe, Mbonimpaye Mpango kushiriki ibada ya misa takatifu katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Anthony wa Padua Jimbo Katoliki Tanga.
Ibada hiyo iliongozwa na Msimamizi Mkuu wa Jimbo hilo, Padre Thomas Kiangio.
“Tusikate miti ovyo, tusiharibu vyanzo vya maji, tusichafue mazingira, hata huko mitaani tunapoishi tuzingatie sana, na hii ni vita kubwa. Mnasikia kule Dar es Salaam sehemu kubwa ya lile jiji halina maji. Jana nimesimama njiani pale Mkata wananchi wanalalamika umeme unakatika lakini ni kwa sababu mabwawa yetu hayana maji,”alisema.
Dk Mpango pia alihimiza wananchi wa Tanga na Watanzania kwa ujumla waitunze amani ya taifa ikiwa ni pamoja na kuwafichua wenye nia mbaya.
“Kwa hiyo niwaombe kutoa taarifa ya watu ambao hamuwajui, wanakuja majumbani kwenu, wanakaa kwenye nyumba za kulala wageni lakini pengine hawana nia nzuri na taifa letu. Kwa hiyo tuwe macho kutunza amani ya Tanzania ambayo tunajivunia kila siku,”alisema.
Aliwashukuru viongozi wa dini kwa kuendelea kuwa chachu ya amani nchini huku akiwasihi waendelee kuwaombea viongozi waongoze taifa kwa hekima ya Mungu.
Makamu wa Rais yupo ziarani mkoani Tanga kukagua shughuli za maendeleo na kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili wananchi katika mkoa huo.
Juzi Rais Samia Suluhu Hassan alisema maeneo mengi nchini yamekuwa na misimu ya mvua isiyotabirika na mengine kukumbwa na ukame kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayochangiwa na uharibifu wa mazingira.
Rais Samia alisema hayo kwenye Jubilee ya miaka 50 ya kazi ya utume na huduma ya Kanisa la Waadventist Wasabato katika Mkoa wa Dodoma.
Alisema yanayotokea leo ni matokeo ya uharibifu wa mazingira kwa kuwa watu wamevikera vyanzo vya maji na wameharibu mazingira.
Rais Samia alitoa mfano wa watu wanaopeleka makundi ya mifugo kunywa maji kwenye mito.
“Ng’ombe 2,000 au 3,000 wakiingia kwenye mto, ng’ombe mmoja anakunywa lita 45 za maji kwa siku, ng’ombe 3,000 watakunywa lita ngapi? Huo mto utabaki kweli? alisema.
Rais Samia alisema uharibifu wa mazingira ukiwamo ukataji miti kwa ajili ya kuchoma mkaa umesababisha miji mingi ikose maji.
“Miti tunayokata ni ya miaka na miaka na matokeo yake ndio tunayaona leo, vyanzo vya maji vimekauka, unyevu nchini haupo, kuna upungufu mkubwa wa vyanzo vya maji kutokana na uharibifu huo…”