MWENYEKITI wa Kamati ya Kitaifa ya Madini ya Tanzanite, Yusuph Money amesema serikali haikufanya makosa kuamua madini hayo ambayo hayajasanifiwa yasiuzwe nje ya mji wa Mirerani mkoani Manyara.
Money alisema hayo jana katika Mji wa Mirerani baada ya kumalizika kwa mkutano wa hadhara uliokuwa ukihutubiwa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo.
Alisema wanaolazimisha madini ghafi ya Tanzanite yauzwe nje ya Mirerani hawana hoja za msingi.
Money alisema serikali imeruhusu madini ya tanzanite yaliyoongezwa thamani yauzwe nje ya Mirerani na ipo katika hatua za mwisho kukamilisha jengo la kufanyia biashara ya madini ya Tanzanite litakalojulikana kwa jina la ‘Tanzanite City’ lenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni tano.
Kuhusu jiwe la tanzanite ambalo bilionea Saninue Laizer aliiuzia serikali alisema katika soko thamani ya madini hayo haizingatii ukubwa ila ubora ikiwamo rangi yake.
“Serikali ilinunua jiwe la tanzanite kwa bilionea Laizer kwa thamani ya jiwe na sio ukubwa wa jiwe na fedha aliyoipata iliendana na ubora wake na sio ukubwa,” alisema Money.
Mbunge wa Jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka alisema uamuzi wa serikali kuhusu soko la madini liwe katika Mji wa Mirerani haukufanywa kwa kukurupuka.
Ole Sendeka alimpongeza Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwaamini wafanyabiashara wa tanzanite na kusogeza huduma ya soko katika Mji wa Mirerani.
Alihimiza wafanyabiashara wa Tanzanite wamuunge mkono Rais Samia katika jitihada za kuhakikisha biashara hiyo inafanyika katika Mji wa Mirerani ikiwa ni pamoja na kulipa kodi stahiki.