Serikali yarudisha 100% ushuru korosho

DODOMA; SERIKALI imeamua kuanzia mwaka huu kurudisha ushuru wa mauzo ya nje asilimia 100 kwenye korosho ikisema fedha hizo ni za wakulima.

Hayo yalibainishwa juzi na Waziri wa Kilimo Hussein Bashe wakati akijibu hoja za wabunge wakati akihitimisha hotuba yake ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Alisema mwaka jana Rais Samia Suluhu Hassan aliruhusu ushuru wa mauzo ya nje asilimia 50 irudishwe kwa wakulima lakini mwaka huu wamekubaliana na Waziri wa Fedha Dk Mwigulu Nchemba ushuru huo utarudishwa kwa asilimia 100 kwenye korosho kwani ni fedha ya wakulima na rais ameshaidhinisha hilo.

Alisema jambo lingine halmashauri zinapokea ushuru wa uzalishaji halafu kuna watu wa kata nao wanachukua Sh 20 kwa kila kilo, Sh 20 inachukua wilaya na mkoa unachukua Sh 10 na kusema zikipigwa hesabu tani 300,000 jumla wanachukua Sh bilioni 50 wakati halmashauri ikishachukua ushuru unatosha.

Bashe alisema kuanzia sasa wanapunguza Sh 10 kutoka kwenye Bodi ya Korosho na Sh 10 kutoka Bodi ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI).

Alimshukuru rais kwa kukubali na kuidhinisha Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo na ilipitishwa sheria mwaka jana na kuwa kazi za mfuko huo ni kuweka mazingira tulivu, kuendeleza miundombinu na kusaidia mifumo ya umwagiliaji na kidijiti.

Alisema Waziri wa Fedha alisaini kanuni kwa ajili ya vyanzo vya fedha na unakwenda kuanzishwa Mfuko wa Kuendeleza Kilimo nchini na utakuwa na jukumu la kutengeneza mazingira tulivu ili bei zinapoanguka katika soko la dunia mkulima alindwe kutokana na bei hiyo.

Kwa mujibu wa Bashe kuna mifumo hiyo kwenye tumbaku, pamba na utatengenezwa kwenye korosho na mazao mengine ili kuwalinda wakulima.

Aliwaomba wabunge watakapokuja kusoma bajeti ya mwakani kutakuwa na tengo lililo wazi la mfuko wa kuwalinda wakulima nchini.

Habari Zifananazo

Back to top button