SERIKALI imesaini mikataba miwili na Kampuni Mbili za Kichina kujenga barabara ya Kilomita 160 ya Mnivata Newala-Masasi mkoani Mtwara.
Ujenzi wa barabara hiyo utagharimu shilingi bilioni 234.512, fedha ambayo imetolewa kama mkopo na Benki ya Maendeleo ya Africa (AfDB). Ujenzi huo utahusisha ujenzi wa daraja la Mwiti.
Mikataba hiyo imesainiwa leo baina ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANRAODS) na Kampuni ya China Wu Yi Company na China Communication Construction Company Limited.
Akizungumza katika hafla ta utiaji saini, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami.
Amesema Kampuni ya China Wu Yi itajenga kilomita 100 sehemu ya barabara hiyo kutoka Mnivata -Mitesa kwa gharama ya shilingi bilioni 141.964, huku Kampuni ya China Communication Construction ikijenga kilomita 60 ya barabara hiyo kutoka Mitesa Hadi Masasi Kwa shilingi bilioni 92.548.
Waziri huyo amesema madhumuni ya ujenzi wa barabara ya Mnivata Newala-Masasi ni kuwaondolea wananchi kero ya usafiri wa barabara na kuboresha mitandao wa barabara ya usafiri na usafirishaji na kukuza uchumi.
“Barabara hii pia ni kiungo muhimu kwa barabara kuu ya kutoka Mtwara mpaka Mbamba Bay inayojulikana kama Ushoroba wa Mtwara, ambayo inaunganisha na nchi jirani ya Msumbiji,” amesema.
Amewataka viongozi wa serikali Mtwara pamoja na wananchi kuwapa ushirikiano wakandarasi walioko kwenye miradi mbalimbali, hususan wakandarasi watakaofanya kazi ya ujenzi wa mradi wa Mnivata Newala-Masasi