Serikali yashauriwa kudhibiti mikopo chechefu

WACHAMBUZI wa masuala ya kiuchumi wamesema kutokana na kuwapo mikopo mingi chechefu katika mifuko 52 ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ni vyema serikali ikaanzisha dirisha maalumu kwenye benki zake ili ziisimamie.

Hivi karibuni Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilibaini kuwapo mifuko 52 ya uwezeshaji wananchi kiuchumi na ambayo uendeshaji wake una upungufu kutokana na kuwapo wa mikopo chechefu na kunufaisha baadhi ya watu wasiostahiki.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Naghenjwa Kaboyoka aliwaeleza wabunge kuwa kuna usimamizi wenye dosari wa mifuko hiyo unaosababisha matumizi mabaya ya fedha za umma.

Advertisement

Kaboyoka alisema ukaguzi ulibaini kuwa, kulikuwa na mikopo chechefu yenye thamani ya Sh bilioni 50.04 toka kwenye mifuko mitatu.

Mfuko wa pembejeo za kilimo ulikuwa na mikopo chechefu ya Sh bilioni 20.1, kati ya Sh
bilioni 27.87 ya fedha zote zilizokopeshwa.

Mwingine ni Mfuko wa Kilimo Kwanza ulikuwa na mikopo chechefu ya Sh bilioni 27.6 kati ya Sh  bilioni 34.2 ya fedha zote zilizokopeshwa, na mfuko wa kutoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo wa SELF ulikuwa na mikopo chechefu ya Sh bilioni 2.7 kati ya Sh bilioni 36.9 zilizokopeshwa.

Rais wa Chama cha Wahasibu Tanzania (TAA), Godvictor Lyimo alisema kuna tatizo la uongozi kwenye mifuko hiyo hivyo ni muhimu kuwapata kwa njia ya ushindani.

“Tukiwa na uwezo mzuri kwenye mifuko, ukopeshaji utazingatia sifa muhimu kwa wakopeshwaji na hili litaondoa tatizo, ni muhimu kuajiri watu wenye uwezo kila eneo, pili wanasiasa wasiruhusiwe kuingilia utendaji wa kazi wa mifuko hii,” alisema Lyimo.

Pia alisema ni vyema wanaokiuka uendeshaji wa mifuko hiyo wakawajibishwa ili kupeleka ujumbe kwa jamii kuwa hakuna uvumilivu kwenye ufisadi.

Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Gabriel Mwang’onda alisema badala ya kuanzisha mifuko hiyo mingi ni vyema zikateuliwa benki zenye vinasaba na serikali kama vile Benki ya Biashara Tanzania (TCB) ili zitumike kuanzisha dirisha maalumu la kuwezesha wananchi.

Mchambuzi mwingine, Walter Nguma alishauri fedha zisipelekwe kwenye halmashauri au manispaa au mifuko hiyo, zipelekwe benki ili wenye sifa wapatiwe mikopo hiyo.

“Kwa mfano tuna Benki ya Maendeleo ya Kilimo, tunaweza kuzipeleka huko ili vijana wanaotaka mikopo ya kilimo waende huko kwa kuwa ni rahisi kwa benki kuliratibu suala hilo kwenye kanzidata inayoeleweka,” alisema Nguma.

Nguma alisema kama serikali itaamua kuzipitisha fedha hizo kwenye benki inabidi ufanyike ukaguzi maalumu naowezwa kufanywa na CAG na kampuni maalumu kutoka nje ili kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwenye malengo yaliyokusudiwa.

Alisema Kamati ya PAC huwa inaibua tatizo hilo kila mara, hivyo ni vyema ikapewa nguvu ya kuwapeleka wahusika kwenye vyombo husika ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

“Unaweza kukuta mikopo chechefu ni asilimia 5 au 2 au 3 au 6, ni mara chache sana kufikia asilimia 10. Hizi asilimia ni ndogo ikilinganishwa na idadi ya watu wanaopata mikopo hiyo, hivyo ni vizuri fedha hizo zikahamishiwa kwenye mabenki,” alisema Mwang’onda.

Aliishauri serikali iwachukulie hatua wahusika kwenye mifuko walioshiri kusababisha kuwapo kwa mikopo chechefu ili watu waogope kuiba fedha za umma.