SERIKALI imeshauriwa kufikiria upya suala la kodi kwenye huduma za kutuma na kutoa pesa kwa njia ya simu wananchi wa vijijini wapate huduma hiyo.
Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya mawasiliano ya Airtel Tanzania, Dinesh Balsingh, amesema hayo leo katika Jukwaa la Kodi na Uwekezaji Tanzania lililoandaliwa na Wizara ya Fedha na Wizara ya Uwekezaji, kwa lengo la kusisitiza jukumu muhimu la teknolojia katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Balsingh pia, aliiomba serikali kufikiria upya kodi kwenye vifaa vya simu hatua ambayo itaongeza kwa kiasi kikubwa kuenea na kukuza matumizi ya simu janja kutokana na kuongozeka kwa matumizi ya huduma za kimtandao ambapo kwa upande mwingine, itaboresha upatikanaji wa huduma mbalimbali kwa jamii.
“Naipongeza serikali kwa kuondoa ushuru wa muda wa maongezi na kupunguzwa kwa kiasi kikubwa cha tozo za ada za mabango, kuanzia Julai 1, 2023 na pia, asilimia 72 ya Watanzania hutumia huduma za pesa za simu, ikionyesha umuhimu wa teknolojia katika kupanua upatikanaji wa huduma za kifedha,”alisema.
Pamoja na hayo, alisema kwamba Airtel Tanzania imefanikiwa kujenga na kuwasha minara mipya 30 ya mawasiliano kati ya minara 758 ambayo ipo kwenye mipango ya utekelezaji kutokana na makubaliano ya serikali na benki ya Dunia kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF) na makampuni mbalimbali ya mawasiliano nchini ili kufanikisha malengo ya kupeleka mawasiliano vijijini.
Alisisitiza umuhimu wa mipango kama msamaha wa VAT kwenye vifaa vya kisasa ili kuziba pengo kati ya miundombinu na matumizi, akikubaliana na ripoti ya UNICEF inayogusia gharama za upatikanaji wa simu za mkononi kama kikwazo kikubwa cha matumizi ya intaneti.
Balsingh aliwahimiza wadau kuendeleza ushirikiano ili kufungua njia nyingi zaidi za teknolojia kutumika kama chanzo cha kukuza usawa na ustawi wa jamii.