Serikali yashauriwa kutafuta mwekezaji TTCL

SERIKALI imeshauriwa kutafuta mwekezaji mwenza katika Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kuiwezesha kuongeza ufanisi na kumudu ushindani wa kibiashara.

Wataalamu na wachambuzi wa uchumi na masuala ya mawasiliano wamesema mwekezaji binafsi ataiwezesha TTCL kujiendesha kisasa na kwa kuzingatia mahitaji ya sasa kwa kuwa mbunifu kulingana na ushindani uliopo.

Baada ya kupokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu (CAG) na ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambaba Rushwa (Takukuru) Rais Samia Suluhu Hassan alisema TTCL imeshindwa kufanya biashara ya simu.

Advertisement

Rais Samia alisema TTCL inaweza kubaki kuusimamia mkongo wa mawasiliano ili wazifuatilie kampuni nyingine za simu na akasema shirika hilo likifanya biashara ya simu kunakuwa hakuna uwanja sawa wa ushindani.

Mtaalamu wa masuala ya mawasiliano, William Kalaghe alisema TTCL inahitaji kujitathmini na kuwekeza katika utaalamu kwa kutafuta watu wenye taaluma sahihi wanaoweza kulifanyia mageuzi shirika hilo ili limudu ushindani kwenye huduma za mawasiliano.

Kalaghe alisema maendeleo ya TTCL katika siku zijazo yanategemea uwekezaji katika sekta ya teknolojia ambayo kimsingi ndiyo inayoonesha na kujenga ubora wa mawasiliano siku zote na kuwavuta wateja katika ulimwengu wa kidigitali.

Alisema mfumo wa huduma kwa wateja wa TTCL si imara ikilinganishwa na na kampuni nyingine za simu na akatoa mfano kuwa kampuni zinazohudumia wateja kwa saa 24.

Mchambuzi wa masuala ya Uchumi ambaye pia ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT), Dk Isack Safari ameshauri serikali ifanye uwekezaji wa kisasa TTCL.

Dk Safari alisema haiwezekani TTCL kuondolewa na kazi zake kuchukuliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kuwa uwepo wa shirika hilo unawezesha utulivu na usalama wa nchi.

Alisema hata kama shirika hilo litaacha kutoa huduma za simu na kuwekeza katika huduma za data kupitia mkongo wa taifa kinachotakiwa ni kufanya uwekezaji wa kisasa kulingana na wakati.

Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Gabriel Mwang’onda alisema ili kuongeza tija TTCL ni lazima serikali iruhusu mwekezaji atayeliendesha shirika hilo katika mfumo binafsi na agawane faida na serikali.

Mwang’onda alisema kinachoisumbua TTCL ni upatikanaji wa watu wanaoweza kuliendesha shirika hilo kwa faida na kwamba, huduma za shirika hilo kwa wateja zimezorota kwa kuwa wafanyakazi hawajitumi.