Serikali yashauriwa mifuko mitatu bima ya afya 

SERIKALI imeshauriwa kuboresha muswada wa bima ya afya kwa wote kwa kuwa na mifuko mitatu ukiwamo wa sekta binafsi isiyo rasmi.

Hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan alisema muswada wa sheria ya bima ya afya kwa wote utawasilishwa kwenye mkutano wa nane wa Bunge unaoendelea jijini Dodoma.

Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Shedrack Mwaibambe alisema ni muhimu serikali ikaunda mamlaka inayojitegemea kusimamia bima ya afya kwa wote.

“NHIF (Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya)  ijigawanye iwe na mifuko mitatu; Mmoja ni wa watumishi wa umma wale ambao ni waajiriwa wa serikali lakini mwingine uwe wa watumishi wa sekta binafsi rasmi na mwingine uwe wa sekta binafsi isiyo rasmi,” alisisitiza.

Aliongeza “Kuwe na mamlaka huru ya kuweza kuongoza mfuko kwani sasa uko chini ya Wizara ya Afya na ina mambo mengi wakati mwingine hili litakuwa la msingi na itatatua matatizo mengi sana.”

Dk Mwaibambe alisema ni muhimu kuwe na mifumo mizuri ya teknolojia ya habari na mawasiliano (tehama) kufuatilia taarifa za mfuko huo yakiwemo matumizi ya fedha.

Alisema miundombinu ya kutambua nani anastahili kupata huduma nani mwenye kadi ni muhimu na unahitajika ubunifu katika kuiendesha mifuko.

“Kadi za vifurushi ilikuwa ni ubunifu mzuri lakini hawakuangalia  mbele kwani wengi wanaokata kadi za vifurushi ni wagonjwa. Sasa unapokuwa  na mfuko wa bima ya afya halafu wengi ni wagonjwa, huo hautakuwa mfuko lengo mzima amchangie mgonjwa unatakiwa kuwa na watu wengi ambao hawaumwi,”alisema Mwaibambe.

Alisema ni muhimu watumishi wanaohudumu katika mifuko kufuatiliwa mienendo yao. “Lakini pia wapitie gharama upya hauwezi kusema mama akijifungua gharama ni shilingi 30,000 ,wanatakiwa wajumlishe gharama ya vifaa kama nyuzi,glovu, nguo ngapi wafanye  majumuisho ,”alisema Dk Mwaibambe.

Alishauri kuwepo na mamlaka huru ya watu kupeleka malalamiko yao endapo hawataridhishwa na huduma na kufanya uchaguzi wa dawa na vifaa tiba wanavyohitaji.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dar es Salaam, Profesa Lawrence Museru alishauri bima ya afya kwa wote iruhusu utoaji wa matibabu yanayohitajika kwa mgonjwa kwa ngazi zote.

“Mfumo wote wa Tanzania kuna ile hatua za chini ambazo zinaweza kutibiwa katika ngazi za chini ambayo gharama zake za huduma ziko chini. Kwa hiyo itakuwa matumizi sahihi ya bima  na  yule ambaye tatizo lake linaweza kutatuliwa juu, apewe rufaa. Ukishasema bima ya afya kwa wote halafu useme huyu asitibiwe hapa wakati anatakiwa kutibiwa pale itakuwa haimsaidii,”alisema Profesa Museru.

Alisema ni muhimu watu waelimishwe faida ya kuwa na bima ya afya na kwamba Watanzania wengi hawawezi kulipa huduma za afya kutoka mifukoni hali inayosababisha serikali kuingia gharama kubwa.

“Unapobaki na madeni katika hospitali  na kila kitu kinahitaji kununuliwa kuanzia dawa na vifaa tiba, maana yake ni kwamba  utashindwa kuendeleza utoaji huduma ambao unakidhi mahitaji  kwa sababu  utashindwa kununua dawa na vifaa tiba vinavyotakiwa na utashindwa kushughulikia vitakapokuwa na matatizo,”alieleza

Daktari bingwa wa uzazi, Colman Gyan alisema huduma zinatakiwa  zilingane kuanzia ngazi ya chini hadi juu ili wananchi waone faida ya bima ya afya kwa wote.

“Mfano daktari bingwa  yuko hospitali ya rufaa na wilaya, mgonjwa aweze kuwaona…, bima  kwa wote ni jambo zuri tunaona wengi wanakata bima wakiwa tayari wanaumwa mwisho wa siku bima inapata hasara,”alisema Dk Gyan.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button