Serikali yashitukia uingizaji mifugo kinyemela nchini

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango amesema ana taarifa mifugo inaingizwa kinyemela katika Mkoa wa Ruvuma na kusababisha uoto wa asili upotee.

Alisema hayo baada ya kushiriki ibada ya Jumapili katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Kiliani, Jimbo Kuu Katoliki Mbinga mkoani humo jana.

Ibada hiyo iliongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Mbinga, John Ndimbo na ilihudhuriwa pia na viongozi wa serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Dk Mpango alisema Mkoa wa Ruvuma umeanza kuharibu mazingira kutokana na kuingizwa ng’ombe kupita kiasi na kukatwa miti.

“Hali ya mazingira si nzuri, tumeharibu ndio maana mvua hazinyeshi vizuri. Bahati Ruvuma bado kuna nafuu lakini kwa taarifa nilizo nazo watu wameingiza ng’ombe kila mahali na mazingira yameharibika, kumbe naambiwa misitu naona tu barabarani lakini ukienda katikati watu wamefyeka miti, uoto wa asili umepotea,”alisema Dk Mpango.

Aliongeza, “kwa hiyo maana yake, uzuri wa Mbinga, uzuri wa Mkoa wa Ruvuma utapotea…tuanze kuchukua hatua ya kupanda miti, miti ya kivuli, miti ya matunda, miti ya mbao, lakini hata maua majumbani kwetu. Ni jambo la msingi sana ili watoto wazuri ninaowaona hapa Mbinga wakue na wao wakiiona Mbinga nzuri.”

Awali, akizindua Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kwa Mkoa wa Ruvuma , Dk Mpango aliviagiza vyombo vya ulinzi na usalama vidhibiti uingizaji wa mifugo kinyume na sheria katika mkoa wa Ruvuma hasa wilaya za Tunduru, Namtumbo na Songea Vijijini.

Alisema mifugo hiyo inamilikiwa na viongozi na matajiri wa mifuho kutoka nchi jirani na inaingizwa katika maeneo hayo kwa kusindikizwa na polisi usiku wa manane.

“Nimeambiwa askari hao wanalipwa kati ya Shilingi 100,000 na 120,000 kwa ng’ombe mmoja kwa hiyo kwa fuso lenye ng’ombe 50 maana yake wanajipatia Shilingi 5,000,00…madhara ya jambo hili ni makubwa sana,”alisema Dk Mpango.

Wakati huo huo alihimiza wazazi na walezi kuweka mkazo wa elimu kwa watoto ili kuwa na taifa lililoelimika.

Alisema alisema serikali inathamini mchango wa watoa huduma za afya kwa kuwa wana mchango katika kuwahudumia wananchi.

Dk Mpango alisema hayo wakati anazindua Jjengo la mionzi la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma.

Alisema serikali itaendelea kuboresha maslahi ya wahudumu wa afya kwa kuhakikisha inaboresha maisha yao na vitendea kazi.

Habari Zifananazo

3 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button