Serikali yashtukia shahada za ‘ujanja ujanja’

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ameitaka bodi mpya ya Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) idhibiti utoaji shahada za uzamili na ile ya uzamivu ili zitolewe kwa waliokidhi vigezo na si vinginevyo.

Akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa bodi hiyo, Profesa Mkenda alisema kuna uigiziaji machapisho kwa wanafunzi wa shahada za uzamili na wa uzamivu (PhD).

“Mna kazi kubwa sana ya kuhakiki ubora wa elimu unaotolewa ili iende sambamba na kudhibiti utolewaji wa shahada za uzamili na shahada ya uzamivu zitolewe kwa waliokidhi vigezo na si vinginevyo,” alisema Profesa Mkenda.

Aliongeza: “Mkiwabaini wataje chuo alichosoma na msimamizi aliyemsimamia ikiwezekana muwatangaze ili kukomesha tabia hiyo. Kama mtu anataka Master’s au PhD afuate sheria zilizopo.”

Alisema bodi hiyo ina kazi kubwa ya kuwezesha na kudhibiti hivyo watumie nafasi hiyo kuifungua nchi katika sekta ya elimu.

“Msimwangalie mtu usoni kachapeni kazi, jambo la muhimu ni kuzingatia sheria na kutenda haki kwani bodi yenu ina kazi kubwa mbili; ya kwanza kuwezesha na pili ni kudhibiti, sasa kazi ya kudhibiti ina lawama sana na lazima mkubaliane hasa pale mnapotaka kutekeleza jukumu la kudhibiti hapo lazima mguse watu…

“Hivyo msiogope kwani kufanya hivyo itasaidia kuongeza ubora katika sekta yetu ya elimu hasa elimu ya vyuo vikuu ambayo ndio mhimili wa taifa,” alisema.

Aidha, alitaka kuangaliwa kwa sifa za wanaoomba kuwa wahadhiri wa vyuo vikuu kwa kutoangalia tu kiwango cha ufaulu (GPA), bali waangalie pia uwezo wao wa kutoa mawasilisho.

Ameitaka kuwezesha vyuo kufanya udahili na kuhakikisha elimu inayotolewa ina ubora na ufaulu uwe mzuri ili kutengeneza taifa lenye watu wasomi wanaokidhi vigezo.

“Bodi iende kusimamia ubora ili kuleta chachu kwenye elimu ya ngazi ya chini kwani wanafunzi wa vyuo vikuu ndio wanakwenda kufundisha wale wa ngazi za chini,” alisema waziri huyo wa Elimu.

Pia ameitaka kuwezesha utambuzi wa vyuo vikuu vya nje ya nchi ikiwezekana kwenda kufanya uchunguzi kuhusu ubora na nafasi ya vyuo hivyo katika nchi zao ili kuwasaidia vijana wa Kitanzania wanapokwenda kusoma nje wasome katika vyuo bora na vyenye ushindani.

Mwenyekiti wa bodi hiyo, Profesa Penina Mlama alisema watatekeleza maelekezo yote ikiwamo kuifungua nchi kimataifa kwa kuwapeleka wanafunzi wengi kusoma vyuo vya nje ya nchi, kuongeza kasi ya udahili, na kusimamia ubora wa elimu inayotolewa na vyuo vikuu.

 

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x