Serikali yasitisha uchenjuaji dhahabu mgodi EMJ Simiyu

SIMIYU: Serikali wilayani Busega Mkoa wa Simiyu, imesitisha shughuli za uchenjuaji wa dhahabu katika mgodi wa EMJ kutokana na wananchi kulalamikia maji yanayotiririshwa kutoka ndani ya mgodi huo kudhaniwa kuwa na sumu.

Mgodi huo wa dhahabu upo mpakani mwa wilaya hiyo na Wilaya ya Bariadi, ambapo wananchi waliolalamika ni kutoka katika kijiji cha Imalamate kilichopo upande wa Wilaya ya Busega.

Hatua hiyo imetangazwa jana na Mkuu wa Wilaya hiyo Faidha Salim, baada ya kukutana na wananchi hao nje ya mgodi huo, ambapo kabla ya kutoa tamko hilo alitembelea maeneo yote yaliyoathiriwa na maji hayo.

SOMA: Samia atoa pole waliokufa migodini Simiyu

Awali akizungumza Diwani wa Kata ya Imalamate Richard Magoti alisema ng’ombe watano, mbuzi mmoja wamekufa kutokana na kunywa maji hayo, huku zaidi ya ngo’mbe 80 wengine walionekana kukosa nguvu baada ya kunywa tena maji hayo.

Alisema kuwa mbali na hilo baadhi ya mashamba ya wananchi ya mchele ya wananchi waliolima karibu na mgodi huo, mazao yao yamekauka kutokana na kuingiliwa kwa maji hayo yanayodhaniwa kuwa na sumu.

“ Haya maji yanatoka ndani ya mgodi huu, yanaonekana kuwa na sumu, yametiririshwa hadi kwenye mto wetu ambao ni tegemeo kwa mifugo yetu na matumizi yetu ya kawaida pamoja na kilimo cha umwagiliaji,” alisema Magoti…

“ Katika huo mto kuna samaki, jana tumeshuhudia idadi kubwa ya samaki wamekufa ndani ya maji, lakini ndege na vyura tumekuwa wamekufa baada ya kunywa hayo maji, mpaka sasa wananchi wangu wako kwenye hatari kubwa ya kupoteza maisha au kupata matatizo ya kiafya,” alieleza Magoti.

Baada ya kuwasikiliza wananchi hao, Mkuu huyo wa Wilaya alisema serikali imemwagiza mwekezaji katika mgodi huo kusitisha mara moja zoezi la uchenjuaji wa dhahabu mpaka vipimo vya maji hayo vitakapomalizika.

Alisema kuwa watalaamu kutoka NEC wameanza kuchukua sampuli za maji hayo kwa ajili ya kufanya vipimo kuangalia kama kweli maji hayo yana sumu na kama ipo ni kwa kiwango gani.

Habari Zifananazo

Back to top button