Serikali yasitisha ujenzi holela vituo vya mafuta

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angelina Mabula ameagiza kusimamishwa kwa ujenzi wa majengo yanayojengwa kinyume cha sheria.

Dk Mabula pia ameagiza kuondolewa vituo vya mafuta vilivyojengwa kinyume cha sheria ikiwa ni pamoja na kutozingatia umbali. Alitaka wabadilishe umbali wa kutoka mita 200 hadi mita 500 wa kituo kimoja kwenda kingine.

Alitoa maagizo hayo jana Dar es Salaam katika kikao kazi na makamishina wasaidizi kutoka mikoa mbalimbali ambapo pia aliagiza makamishna wa wizara waliotoa vibali bila utaratibu wachukuliwe hatua.

“Tumeendelea kushuhudia ongezeko la ujenzi holela na viongozi wapo na miji inazidi kuharibika. Majengo yanajengwa lakini hayapo kwenye masterplan. Mkasimamie hilo, majengo yanayojengwa kinyume na taratibu yasimamishwe haraka,” alisisitiza.

Aliongeza: “Kumezuka vituo vya mafuta kila kona. Ilikuwa mita 200, badilisheni iwe mita 500 kwani ikitokea moto umewaka ni hatari sasa. Vituo vinajengwa kila sehemu bila udhibiti na nyie mnaangalia,” alisema.

Dk Mabula pia alieleza kukasirishwa na utendaji wa kazi mbovu na kutokuwa na ushirikiano baina ya makamishina wa ardhi na viongozi wengine. Dk Mabula pia alimwelekeza Katibu wa Wizara hiyo kuhakikisha anaanza kuchukua hatua mara moja kwa makamishna wasaidizi wa ardhi wale walioshindwa kukidhi matarajio pamoja na wasaidizi wao.

Alisema makamishina hao wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea, wanaogopana, wanalindana na hivyo kuathiri utendaji wa kazi.

“Mikoa ambayo tunakamilisha taratibu za kinidhamu kwa watumishi siku za hivi karibuni ni Mbeya, Dar es Saaam, Mwanza na Arusha na Lindi,” alisema.

Alisema pamoja na hatua za kinidhamu ambazo zimechukuliwa kwa watumishi ikiwa ni pamoja na kuwaachisha kazi kwa Mkoa wa Mbeya watatu na Dodoma wanne, ameagiza hatua zichukuliwe kwa mikoa mingine.

Habari Zifananazo

Back to top button