Serikali yataja mambo matano kusimamia bajeti

SERIKALI imetangaza mambo matano inayozingatia kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa mipango na bajeti zinazopitishwa.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Chande alitangaza hayo bungeni Dodoma jana wakati anajibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Nusrat Hanje. Mbunge huyo alihoji serikali inatumia utaratibu gani kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa mipango na bajeti zinazopitishwa.

Chande alisema kila mwaka Wizara ya Fedha na Mipango huandaa na kusimamia utekelezaji wa Mwongozo wa Maandalizi na Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Serikali.

Aliwaeleza wabunge kuwa serikali pia hutoa waraka namba moja wa mwaka wa fedha wa utekelezaji wa bajeti unaoelekeza na kusisitiza utekelezaji wa vipaumbele.

Chande alisema pia serikali inatekeleza hilo kwa kuandaa mwongozo wa maombi na utoaji fedha kwa lengo la kuhakikisha fedha inatolewa wakati wa uhitaji na inatumika kwa wakati.

Alisema wizara hiyo inasimamia uwasilishwaji wa taarifa za utekelezaji wa mipango na bajeti ambazo huchambuliwa ili kutathmini utekelezaji wa mipango kwa kuoanisha na malengo tarajiwa na bajeti zilizotengwa.

“Serikali inakitumia ipasavyo kitengo hiki cha ukaguzi wa ndani na tumekiongezea uwezo mwaka huu uliopita na mwaka huu ujao tumetenga kuongeza uwezo tufanye ukaguzi unaostahili,” alisema Chande. Wakati anajibu maswali ya nyongeza ya wabunge, alisema serikali itaendelea kukusanya na kuongeza uwezo wa ukusanyaji mapato ili kutekeleza bajeti kama ilivyopangwa.

Chande alisema pia serikali inabainisha viashiria hatarishi vya utekelezaji wa bajeti na kufanya ufuatiliaji na tathmini ili kujiridhisha na uhalisia na kuchukua hatua stahiki.

Wakati anawasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka wa fedha 2023/2024, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba aliwaeleza wabunge kuwa utekelezaji wa bajeti hiyo unaweza kuathiriwa na vihatarishi yakiwamo mabadiliko ya kiwango cha mfumuko wa bei.

Dk Mwigulu alitaja vihatarishi vingine ni mabadiliko ya viwango vya kubadili fedha na riba katika masoko ya fedha ndani na nje ya nchi, madeni sanjari na mabadiliko ya sera za kibajeti, misaada na mikopo.

“Vihatarishi vingine ni pamoja na mabadiliko ya tabianchi na majanga asilia kama vile matetemeko ya ardhi na magonjwa ya mlipuko,” alisema.

Alitaja athari zinazoweza kujitokeza endapo vihatarishi vya mwenendo wa uchumi jumla na utekelezaji wa bajeti vitatokea ni pamoja na kuongezeka kwa nakisi ya bajeti, kutokufikiwa kwa lengo la ukusanyaji wa mapato, kasi ndogo ya utekelezaji wa miradi na kuongezeka kwa gharama za bidhaa, malighafi, huduma na utekelezaji wa miradi.

Habari Zifananazo

2 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button