SERIKALI imekitaka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), kusimamia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya kiuchumi Ndaki ya Tiba (HEET) utakaojenga Kampasi ya Mloganzila na Kigoma Ujiji, ili kuongeza idadi ya wanafunzi wa elimu ya juu kwa asilimia 30.
Mkurugenzi wa Elimu ya Juu, Profesa Peter Msofe amesema hayo leo Novemba 16, 2023 jijini Dar es salaam wakati akifungua kongamano la miaka 60 ya MUHAS kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda.
Amesema uanzishwaji wa ndaki hiyo unaendana na maono ya chuo ya kufanya mageuzi na kuwa mji wa taaluma za afya kufikia 2050.
“Ni imani yangu mtaendelea kutekeleza mradi kwa kuzingatia ratiba na malengo mliojiwekea kwa kuzingatia viwango vya serikali na Benki ya Dunia,” amesema Prof. Mkenda na kuongeza kuwa:
“Mradi huu ukisimamiwa utaongeza idadi ya wanafunzi wa elimu ya juu kwa asilimia 30 katika maeneo 14 ya kipaumbele kwa uchumi wetu wa kati wa viwanda,”amefafanua Prof. Mkenda.
Pia amewasisitiza kuzingatia rasilimali zilizopo kwani serikali inaboresha uchumi kwa kuleta mapinduzi ya viwanda na kuhakikisha maisha na afya za wanafunzi zinaboreshwa.
Akizungumzia kuhusu tafiti, Prof. Mkenda amesema, chuo hicho kinaongoza kwa tafiti nyingi za afya nchini na kwamba zimeweza kuleta mapinduzi kwenye sera na miongozo inayotumika ndani na nje ya nchi hususan katika kuboresha huduma za afya, kutoa matibabu sahihi na kuzuia magonjwa.
Amesema tafiti hizo zimechangia kukiweka chuo katika nafasi nzuri kwenye uanzishwaji wa vyuo vikuu bora nchini, barani Afrika na duniani kwa ujumla na kwamba ukuaji wa vyuo vikuu Tanzania hususan vinavyotoa elimu na kufanya tafiti za afya ni miongoni mwa mafanikio makubwa ambayo nchi inaendelea kujivunia katika sekta ya elimu na afya.
Amesema kuwepo kwa nia thabiti ya serikali na sera rafiki, imechangia kuwa na vyuo 13 vya serikali vinavyotoa mafunzo ya shahada mbalimbali za afya ikiwa ni pamoja na udaktari.
“Ongezeko hili limesaidia kuongeza wataalamu katika sekta ya afya ambayo bado inakumbwa na uchache wa wataalamu. Tangu chuo kianzishwe kimezalisha wataalamu wa afya 20,000 kwa ngazi ya shahada ya awali na wataalamu bingwa 4,200 wa ngazi ya uzamili na uzamivu,” amesema Profesa Mkenda.
Kwa upande wa Profesa Appolinary Kamuhabwa, Kaimu Makamu Mkuu wa MUHAS, amesema katika miaka ya 1960 magonjwa makubwa yaliyokuwa yakiikabili nchi ni pamoja na malaria, kifua kikuu, Ukimwi na Virusi Vya Ukimwi.
Amesema miongozo iliyotolewa kuhusu matumizi ya dawa na namna ya kuhudumia wagonjwa hao zimetokana na tafiti walizozifanya na washirika wengine hivyo, zimeboresha sera.
“Kwa sasa magonjwa yasiyo ya kuambukiza ndio yameshika kasi kama kisukari shinikizo la damu, moyo na figo hivyo majibu ya tafiti zetu ndio tegemeo na pia inatupa muongozo katika mitaala yetu,” amesema.
Amesema matokeo ya utafiti ambazo zimefanyika chuoni yamekuwa na mchango mkubwa katika kupata ufumbuzi wa matatizo mbalimbali ya afya yanayoikabili jamii.
“Tafiti zimesaidia kuboresha sera na miongozo ya matibabu na kuboresha huduma na mifumo ya afya. Watafiti wa Muhas wamekuwa vinara nchini na duniani kutokana na ubora wa tafiti zao na mchango mkubwa waliouonesha katika ubobezi wao,” alisema Profesa Kamuhabwa.
Amesema chuo hicho kimeongeza idadi ya shahada za uzamili hadi kufikia 84 na kinaendelea kutoa kipaumbele na kuandaa wanafunzi wa shahada za uzamivu ambao ndio msingi wa tafiti.
Kwa upande wake, Mkuu wa Ndaki ya Afya na Sayansi Shirikishi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Projestina Muganyizi amesema chuo hicho kimepiga hatua katika kufanya tafiti kwani kina wanataaluma zaidi ya 400 ambao wanafanya utafiti.