Serikali yataka tathmini mashirika ya vijana

yanyooshea kidole mashirika 32

SERIKALI imeagiza ofisi ya Msajili wa Mashirika yasiyo ya kiserikali kufanya tathmini ya kina ya kiutendaji kwa mashiriki yasiyoyakiserikali yanayojihusisha na shughuli za vijana.

Agizo hilo limetolewa jijini Dodoma  na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Patrobas Katambi wakati wa kongamano la vijana  na kuzinyooshea kidole asasi za kiraia 32 zinazojihusisha na masuala ya vijana.

Amesema ni vyema Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo na Msajili kuzifanyia tathmini ili kujua utendaji kazi wake lengo likiwa zinajulikana zinafanya nini ili kuona kama zinakidhi tija na haja ya vijana na kama kuna vikwazo dhidi ya asasi hizo.

“Hizi asasi zifanyiwe tathimni ya kina ili kujua kama zinakidhi tija na haja ya vijana wa taifa hili au ni kwa maslahi ya wachache, hivyo ni lazima tuzitambue zinazowagusa vijana, maana lisije kutokea baya tukawa na asasi inayoweza kuwa na mafunzo kwa vijana wetu ambayo hayaendani na maadili ya kitanzania.”Amesema Katambi

Amesema, serikali inaandaa Mfumo wa Taifa wa uratibu na tathmini wa afua za masuala ya maendeleo ya vijana nchini ambao utasaidia kuwatambua na kuwaratibu wadau wote.

Aidha, Katambi amesema serikali inatambua umuhimu wa vijana na kuweka kipaumbele katika mipango ya vijana ikiwamo sera ya fedha inayosaidia vijana waliomaliza vyuo vikuu kukopeshwa ndani ya halmashauri zote 184.

Amesema kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana unaosimamiwa na wizara yake kwa mwaka 2022/23 imetoa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni Sh3.2 kwa shughuli za uzalishaji mali na miradi ya vijana 149 yenye vijana 978 katika sekta za kilimo, viwanda, usafirishaji, biashara na huduma.

Pia Serikali imefungua dirisha linalounganisha vijana kwenye fursa za ajira ndani na nje ya nchi kupitia taasisi ya TAESA na kuingiza mazungumzo na nchi nane za Afrika, Qatar, Israel na Marekani.

Awali, Mkurugenzi wa Taasisi ya Maendeleo ya Vijana mkoani Dodoma (DOYODO), Rajab Juma aliiomba serikali kuzitengea ruzuku asasi zinazojihusisha na masuala ya vijana kama ilivyo kwa vyama vya siasa ili kuwafikia kundi kubwa la vijana katika kujenga kesho yao.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Freedom House, Daniel Lema, amesema bado kuna kundi la vijana wanashindwa kutumia fursa zinazowazunguka ili kutengeneza kipato na kuishia kulalamika huku Mkurugenzi wa Foundation For Civil Society, Francis Kiwanga, akisema lazima vijana wahamishe akili zao kutoka kwenye kulalamika na kutembea na vyeti wakisaka ajira, badala yake watafute fursa zinazowazunguka.

Habari Zifananazo

6 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button