Serikali yataka ubunifu kuendesha mashirika

MSAJILI wa Hazina, Nehemiah Mchechu ameagiza wenyeviti wa bodi za wakurugenzi za taasisi, mashirika ya umma na wakala za serikali 298, wawe wabunifu na wabadili fikra katika kusimamia taasisi hizo zilete matokeo chanya kwa manufaa ya taifa.

Pia, ameainisha vigezo zaidi ya 100 vitakavyotumiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) kupima utendaji wa taasisi hizo kulingana na namna zitakavyogawanywa kisekta, kifedha na kiuendeshaji.

Mchechu aliyasema hayo Dar es Salaam jana alipozungumza na taasisi zaidi ya 136 zisizo za kibiashara kuhusu namna ya kuongeza ufanisi wa taasisi hizo.

Mkutano huo ulikuwa na kaulimbiu ‘Kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa taasisi na mashirika ya umma kuelekea uwekezaji wenye tija kwa taifa.’

Mchechu aliwataka wenyeviti hao watambue kuwa taasisi hizo ndio kichwa cha biashara cha serikali na zinapaswa kutoa gawio na endapo kuna mwenyekiti anayeona taasisi yake imeshindwa kufanya hivyo, aachie kiti chake wachukue wanaoweza.

“Wizara zilizopo hazifanyi biashara sisi tunatakiwa ndio tuwe kichwa cha biashara hivyo tubadili thinking (fikra) zetu, lazima tukubaliane tuangalie wapi tuboreshe, tufanye nini. Muhimu tuwe na malengo ya kifedha,” alisema Mchechu.

Alisema mchango wa taasisi hizo serikalini hauridhishi na kuzitaka bodi zilizo kwenye orodha ya taasisi zilizokuwa zinachangia gawio na sasa zimeacha, kujitathmini kwa kuangalia zimekwama wapi na kutafuta suluhu na endapo zitaona imeshindikana zijiondoe zenyewe.

“Kama unaona huwezi tupishe usiendelee na safari au la ibane menejimenti yako metokeo yaonekane,” alisema.

Aidha, alizitaka taasisi ambazo zinaitegemea zaidi serikali na haziwezi kutoa gawio, nazo kuwa wabunifu na kutafuta vyanzo mbadala vya mapato ili kupunguza utegemezi na endapo kuna zinazoona zinaweza kujitegemea zinaruhusiwa kujiondoa kabisa kwenye utegemezi na serikali itazipa ushirikiano.

Alisema katika eneo la ufanisi na utendaji ndio maana kuna kipengele cha taasisi hizo kuingia mkataba na Hazina, ambako kati ya taasisi 248 zilizopo, 236 tayari zimeingia mkataba.

Alisema takwimu alizonazo zinaonesha yapo mashirika na taasisi za umma zinazohitaji mtaji kutoka Hazina unaofikia Sh trilioni 1.1 wakati Bajeti ya Hazina ya Uwekezaji ni Sh bilioni 600 na kusisitizia umuhimu wa ubunifu wa taasisi ili kupunguza mzigo kwa serikali.

“Nasisitiza bodi kuwa na utawala ulio imara na kuzingatia mwongozo wa uwekezaji katika eneo la utendaji wa taasisi ili zizalishe, tusiishie tu kuwekeza bila kupata chochote.

“Pia Hazina tutakuwa na bodi ya ushauri yenye wataalamu waliobobea katika biashara. Tukiyafanya haya ndani ya miaka miwili au mitatu ijayo kutakuwa na mabadiliko makubwa,” alieleza Mchechu.

Akizungumzia vigezo vitakavyotumika kupima utendaji wa taasisi hizo, alisema wameandaa mifumo sahihi ya udhibiti wa utendaji kuhakikisha taasisi na kampuni ambazo serikali ina hisa chache zinajiendesha kwa tija.

Alisema ofisi imeainisha vigezo vya kupima utendaji wa taasisi na kampuni vilivyogawanywa katika makundi matatu ambayo ni vigezo vya kifedha vipo 24; vigezo vya kisekta vipo 69; na vigezo vya uendeshaji vipo 55.

Alitaja maeneo yatakayotumiwa kupima utendaji wa taasisi hizo kuwa ni faida, ukwasi, ufanisi, uendelezaji na fedha.

Alizitaka taasisi hizo kutangaza mazuri na sio kusubiri kuzungumziwa kwenye mabaya tu na kubainisha kuwa ifikapo mwakani itakuwa ni lazima kwa taasisi hizo kutoa taarifa za ripoti zao za utendaji za mwaka kwa umma.

 

Habari Zifananazo

Back to top button