Serikali yatenga milioni 757 ujenzi gereza Kilosa
SERIKALI imetenga Sh milioni 757 kumalizia ujenzi wa gereza jipya linalojengwa wilayani Kilosa ,mkoani Morogoro baada ya gereza la zamani kupitiwa na Reli ya kisasa (SGR).
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Yussuf Masauni alisema hayo Februari 20,2023 kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa Mji Mdogo wa Mikumi, Kilosa.
Masauni ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa gereza hilo jipya katika eneo la Mkono wa Mara , kata ya Chanzuru wilayani humo na kupongeza kazi zinavyoendelea kufanyika.
“ Ujenzi umeanza tayari na kazi inaenda vizuri , huu ni mfano mzuri wa kazi za serikali na inaendeleza miradi mingine mbalimbali ambayo ipo kwenye hatua nzuri za ujenzi wake” amesema Masauni.
Masauni pia amesema serikali katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2022/2023 imetenga fedha za kutosha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya polisi na nyumba za askari wa vyombo vyote vya usalama vilivyopo chini ya wizara hiyo.
Waziri Masauni amesema mpango huo ni wa miaka 10 na kutokana na kasi ya Rais , Dk Samia Suluhu Hassan , utakwenda kumalizika kwa kipindi kifupi kijacho.
“ Lengo letu wizara ni kujenga vituo vya Polisi maeneo mbalimbali nchini ikiwemo na hapa Mikumi na pia ujenzi wa nyumba za askari wa vyombo vute vya ulinzi vilivyopo katika wizara hii na zaidi ya nyumba na vituo vya Polisi 51,780” amesema Masauni
Mbali na hayo akiwa katika gereza la Kiberege na Idete wilayani Kilombero Waziri huyo kuzungumza na maofisa na askari amelipongeza jeshi hilo kwa kuongeza uzalishaji wa mazao ya mahindi na mpunga kwa kutumia utaalamu katika kilimo kwenye eneo dogo na kuvuna mazao zaidi.
Mkuu wa Gereza Msaidizi Gereja la Kiberege, Uswege Yoram amesema uzalishaji wa mazao kwa msimu wa 2021/2022 walivuna gunia 290 ya mahindi na 284 ya mpunga ambapo chakula hicho kilitumika kulisha wafungwa wa gereza hilo na mchele ulisafilishwa kwenda gereza la Tanga na Dodoma kulisha wafungwa.
Yoram amesema kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2022/2023 gereza limelima ekari 200 zao la mpunga ,ekari 100 zao la mahindi na ekari 143 za miwa na mazao hayo yanaendelea vizuri.
Amesema matarajio ya gereza hilo kwa msimu wa 2022/2023 ni kuvuna gunia 1,600 kwenye shamba la mbunga na gunia 800 shamba la mahindi.
Yoram amesema kwa mavuno ya msimu uliopita katika zao la miwa , gereza lilivuna tani 194.2 za miwa na kwa msimu wa mwaka huu mavuno yanaweza kuongezeka mara dufu.