WAKATI Hospitali ya Rufaa ya Kitete mkoani Tabora ikikabiliwa na upungufu wa madaktari bingwa 11, serikali imesema imetenga shiling bilioni nane kwa ajili ya kusomesha madaktari bingwa.
Mbunge wa Tabora Mjini Emmanuel Mwakasaka amesema hospitali hiyo ambayo inategemewa na Wananchi wa mkoa nzima ina madaktari bingwa watano.
Akizungumza katika kipindi cha maswali na majibu, Mwakasaka alihoji ni lini changamoto ya ukosefu wa Madaktari Bingwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kitete itatatuliwa?
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel amesema hadi sasa serikali imepeleka madataktari watano katika Hospitali hiyo ya rufaa ya Mkoa wa Kitete
“Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Kitete hadi sasa ina jumla ya madaktari bingwa watano, ambapo daktari bingwa wa Afya ya akina mama na uzazi ni mmoja, madaktari bingwa wa watoto watatu na Daktari bingwa wa upasuaji mmoja.”Amesema Mollel
Amesema katika kuongeza idadi ya madaktari Bingwa, serikali imepeleka kusoma jumla ya madaktari sita kutoka hospitali ya Rufaa ya Kitete ambao madaktari wawili wanasomea ubingwa wa magonjwa ya ndani, daktari wa magonjwa ya Kinywa, Sikio na Koo mmoja, Ubingwa katika Mionzi mmoja, ubingwa katika magonjwa ya dharura mmoja, na daktari bingwa wa Afya ya akina mama na uzazi mmoja.
Akitoa ufafanuzi zaidi, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema serikali kupitia program maalum ya ‘Samia Super Specialist’ imepanga kusomesha madakatari bingwa 400 .
“Tunapopeleka madaktari bingwa tunapeleka seti nzima mfano wa mifupa, tutampeleka wa mifupa, wa usingizi, muhudumu na wote wanaohitaji kwenye kitengo husika.”Amesema
Aidha, Spika wa Bunge amemshauri Ummy hao madaktari na wahudumu wanaosomeshwa kupitia mfuko huo wawekewe sheria kali itakayowalazimu kurejea maeneo yao ya kazi pindi wamalizapo shule ili kuziba upungufu uliopo.
“Haiwezekani mkawa mnawasomesha alafu wakimaliza hawarudi kule mlipowatoa wanaenda maeneo mengine, kule upungufu unaendelea kuwepo mkubwa, warudi kutumika huko mnapowatoa.”Amesema Tulia