Serikali yatoa bil 160/- kujenga madarasa 8,000

SERIKALI imetoa Sh bilioni 160 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 8,000 vitakavyopokea ziada ya wanafunzi zaidi ya 400,000 wa Kidato cha Kwanza mwakani ambao ni zao la elimumsingi bila ada.

Aidha, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-Tamisemi, Dk Charles Msonde ameelekezwa kufanyia kazi malalamiko ya baadhi ya walimu walioajiriwa hivi karibuni ya kutolipwa posho ya kujikimu.

Haya yameelezwa jijini hapa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2023.

Bashungwa alisema fedha hizo tayari zimeshaingia kwenye akaunti za shule za sekondari 2,439 zilizoainishwa kuwa na upungufu wa vyumba vya madarasa kwa ajili ya Kidato cha Kwanza mwakani.

Alisema kwa sasa fedha hizo zimeshatumwa na kupokelewa kwenye halmashauri zote 184, kulingana na upungufu uliowasilishwa na kila halmashauri husika.

Alisema kwa mwakani takribani wanafunzi 1,148,512 wanatarajiwa kujiunga na Kidato cha Kwanza ambao ni wale walioanza Darasa la Kwanza mwaka 2016 kipindi ambacho serikali ilianza utekelezaji Sera ya Elimumsingi bila ada Desemba mwaka 2015.

“Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi, idadi ya wanafunzi walioandikishwa Darasa la Kwanza ilikuwa kubwa sana, kwa kulinganisha na miaka iliyotangulia. Kwa muktadha huo, wanafunzi waliopo Darasa la Saba mwaka 2022, ndio zao la kwanza la matokeo ya Elimumsingi bila ada,” alisema Bashungwa.

“Hali halisi inajionesha wazi kuwa idadi ya wanafunzi wanaoingia Kidato cha Kwanza ni wengi kuliko idadi ya wanafunzi 454,902 wanaomaliza Kidato cha Nne mwaka 2022.”

Alisema katika hali ya kawaida matarajio ni kuwa nafasi zilizopo kwa ajili ya wanafunzi wanaojiunga na Kidato cha Kwanza, zitokane na uwepo wa shule mpya za sekondari, ujenzi wa miundombinu mipya na nafasi zilizoachwa na wanafunzi wanaohitimu Kidato cha Nne.

“Kutokana na ongezeko la wanafunzi wanaotarajia kujiunga na Kidato cha Kwanza kuwa kubwa ukilinganisha na nafasi zitakazoachwa, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia kutoa kiasi cha shilingi bilioni 160 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 8,000 vitakavyoweza kutosheleza kupokea wanafunzi zaidi ya 400,000,” alisema waziri huyo wa Tamisemi.

Idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka huu ilikuwa ni 907,802 ikilinganishwa na 422,403 waliohitimu Kidato cha Nne, hivyo kuhitaji kuongezeka miundombinu ya madarasa na vyoo yenye kutosheleza wanafunzi 485,399 wa ziada.

Ili kutatua changamoto hiyo, Serikali ya Awamu ya Sita ilitoa kiasi cha Sh bilioni 240 zilizofanikisha ujenzi wa madarasa 12,000, shule shikizi 3,000 na mabweni 60.

Bashungwa alisema pamoja na fedha za ujenzi wa madarasa mapya 8,000, serikali katika mwaka wa fedha 2021/22 ilitoa Sh bilioni 108 kujenga shule mpya za kata 231 ambazo ziko katika hatua mbalimbali za ukamilishaji na zikikamilika zinatarajia kupokea wanafunzi Januari.

Amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya kufuatilia ujenzi huo wa vyumba vya madarasa na kuhakikisha ujenzi unakamilika ndani ya miezi miwili na nusu kuanzia jana.

Katika hatua nyingine, ameagiza kufuatiliwa kwa malalamiko yanayotolewa na baadhi ya walimu 9,800 walioajiriwa hivi karibuni kwenye baadhi ya wilaya kutolipwa posho za kujikimu na huku waliolipwa hawajaoneshwa mchanganuo.

Habari Zifananazo

Back to top button