SERIKALI imesema hapa Tanzania hakuna mgonjwa wa ebola na imetoa maagizo kwa waganga wakuu wa mikoa na halmashauri na wananchi kuchukua hatua za tahadhari dhidi ya ugonjwa wa ebola ambao umeelezwa kulipuka nchi jirani ya Uganda.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu taarifa za mlipuko wa ugonjwa huo ambapo mgonjwa amefariki wilayani Mubende.
Dk Mollel aliagiza waganga wakuu wa mikoa na halmashauri waimarishe utoaji elimu, ufuatiliaji wa ugonjwa, uchunguzi wa kitaalamu na kuhakikisha upatikanaji wa vifaa tiba na kinga muhimu katika maeneo yao.
Pia aliwaelekeza kuimarisha uchunguzi wa wageni wanaoingia nchini kupitia mipaka yakiwemo matumizi ya vipima joto.
Dk Mollel alisema uwepo wa ugonjwa huo Uganda unaiweka Tanzania katika hatari kutokana na mwingiliano wa watu kupitia mipaka ya nchi kavu, viwanja vya ndege na bandari.
Alisema dalili kuu za ugonjwa huo ni pamoja na homa kali, inayoambatana na kutokwa damu katika matundu ya mwili yaani pua, njia ya haja kubwa na ndogo, mdomoni, masikioni na machoni, hali inayopelekea kifo kwa muda mfupi.