WAZIRI wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar, Rahma Kassim Ali, amewataka wakazi wa nyumba za maendeleo kuhakikisha wanalipa kodi, ipasavyo ili kuiwezesha serikali kufikia malengo iliyojipangia.
Akizungumza katika ziara aliyoifanya kwenye nyumba za maendeleo eneo la Kikwajuni, amesema kitendo kinachofanywa na baadhi ya wakazi kutolipa kodi, kimekuwa kikirudisha nyuma jitihada za kuleta maendeleo nchini, kwani kwa sasa zimechakaa na zinahitaji matengenezo.
“Kodi tunayolipa ndio inaliwezesha shirika kuweza kuzifanyia matengenezo nyumba hizo, hivyo tulipe kodi ili twende sambamba na dhamira ya serikali yetu katika kutoa huduma bora kwa jamii,” amesema.
Amesisitiza kuwa suala la kulipa kodi ni lazima kwa kila mkazi ambaye ameingia mkataba na Shirika la Nyumba, lakini pia inaiwezesha serikali kuweza kuzifanyia ukarabati nyumba hizo, ambazo kwa sasa zimechakaa.
Katika hatua nyingine amesikitishwa na kitendo cha baadhi ya wakazi wake kutupa taka ovyo na kuzifanya kuwa katika hali ya uchafu, kitendo ambacho kinaikosesha muonekani mzuri wa nyumba hizo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu Shirika la Nyumba, Mwanaisha Ali Saidi amesema kwa sasa shirika hilo linatafuta wawekezaji, ili kuona namna ya kuweza kuzifanyia matengenezo nyumba hizo ambazo nyingi zimeonekana kuchakaa na kutokua katika hali nzuri.
Amewataka wakazi pindi wanapotaka kufanya matengenezo katika nyumba hizo, kuomba kibali cha kufanya hivyo kwa mujibu wa taratibu na sheria zilizowekwa.
Nyumba za maendeleo kikwajuni zipo 190, ambapo nyumba 89 ni za serikali na zinasimamiwa na Shirika la Nyumba la Zanzibar na nyumba 101 ni za watu binafsi, ambazo walipewa fidia kwa kubomelewa nyumba zao wakati wa kujengwa nyumba hizo.