Serikali yatoa msaada waathirika wa mafuriko

SERIKALI imetoa msaada wa mahitaji mbalimbali kwa waathirika wa mafuriko yaliyosababishwa na mvua iliyonyesha ya Januari 7, 2023 Jijini Mbeya na kusababisha athari ikiwemo uharibifu wa miundombinu na mali za Wananchi.

Kwa niaba ya Serikali, Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene akiambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mbeya na Mbunge wa Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson, leo Januari 11, 2023 amekabidhi misaada hiyo kwa uongozi wa mkoa huo ikiwemo tani 50 za mahindi, magodoro 300, mablanketi 1200, mikeka 550, madumu ya maji 600, sufuria, vikombe, sahani n.k

Simbachawene amewaeleza Wananchi hao kuhusu hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali ikiwa ni pamoja na maelekezo waliyopewa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan ya kuwataka kuboresha miundombinu ya Jiji hilo pamoja na kuwahudumia waathirika hao chakula kwa kipindi cha miezi mitatu mfululizo.

Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amewataka Wananchi kuwa watulivu katika kipindi hiki wakati Serikali ikiendelea na jitihada za kuwahudumia pia amewatahadharisha kuepuka kujenga makazi katika maeneo ambayo sio rasmi na hatarishi.

Mbunge wa Mbeya Mjini ambaye pia ni Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson ameishukuru Serikali kwa kuchukua hatua za haraka katika kuwasaidia Wananchi wake na zaidi ameiomba kulitazama kwa upekee Jimbo hilo ambalo limekuwa na changamoto nyingi za miundombinu.

Habari Zifananazo

Back to top button