Serikali yatoa tamko, kuhamisha wananchi Ngorongoro
DODOMA: Serikali imesema siku chache zijazo itaendelea na awamu ya pili ya shughuli ya kuwahamisha kwa hiari wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro wilayani Ngorongoro mkoani Arusha, wanaoishi ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.
Akitoa taarifa hiyo leo Desemba 15, 2023 Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi amesema shughuli hiyo ni kwa wananchi waliotayari na waliokwisha kujiandikisha.
“Serikali inarudia kusisitiza tena, zoezi hili ni la hiari na hakuna haki za binadamu zinazovunjwa na linafanyika kwa faida ya wananchi wenyewe ambao ni raia wa Tanzania wanaostahili usalama na maendeleo pamoja na hifadhi ambayo ni urithi wa taifa hili na dunia nzima.
Aidha ameongeza kuwa Serikali inasisitiza pia wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro waliopo Lolindo hawafukuzwi kwenye maeneo yao bali serikali ilikubali kuwaachia eneo la Km za mraba 2,500 na kubakia na Km za mraba 1,500 ambazo ni kwa ajili ya hifadhi ya misitu, vyanzo vya maji, wanyama na ni sehemu muhimu ya mfumo wa ikolojia wa Serengeti na Maasai Mara unaojumuisha mzunguko wa wanyama – kuhama kwa wanyama.
Matinyi amesema kuwa Serikali iko tayari kuwapokea wataalamu wa UNESCO wanaokuja kuangalia jinsi zoezi hili linavyokwenda ikiwemo kukagua uhifadhi wa Ngorongoro.
“Wataalamu hawa watakuja Januari 2024. Serikali inatambua kwamba jumuiya na asasi mbalimbali za nje ya nchi zinaweza zikatoa maoni yao kwa kadri zinavyofahamu lakini ni muhimu wahusika wote wakatafuta ukweli ikiwemo kuja nchini kwa kupanga vema na serikali. Serikali ina uhusiano mzuri na EU na hivi karibuni Kamishna wa EU, JANEZ LENARCIC, aliielezea Tanzania kama mshirika wa kimkakati na ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na EU unaendelea kuimarika” amesema Msemaji Mkuu wa Serikali.