SERIKALI imetoa wito kwa watoa huduma kuendelea kuwatambua kuwatambua wateja wanaotumia vitambulisho vya taifa (NIDA) vyenye tarehe za ukomo hadi pale maelekezo mengine yatakapotolewa.
Akizungumza bungeni, Dodoma leo asubuhi kwa niamba ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis amesema zaidi kwamba Namba za Utambulisho (NIN) zilizopo katika vitambulisho hivyo hazina ukomo wa muda wa matumizi.
“Aidha, marekebisho hayo hayatahusu muda wa matumizi ya Vitambulisho vya Taifa kwa Wageni Wakaazi (Legal Residents) na Wakimbizi,” amesema Naibu Waziri wakati akijibu swali la msingi la Mbunge Dorothy Kilave.
Katika swali hilo lililoulizwa kwa niaba yake na Mbunge Jenny James, Dorothy alitaka kufahamu tamko la Serikali kuhusu kitambulisho cha taifa kuwekwa ukomo wa kutumika.
“Vitambulisho vya Taifa vilivyotolewa hadi mwaka 2022 vilikuwa na tarehe ya ukomo wa kutumika (Expiry Date). Serikali imefanya marekebisho ya Kanuni za Usajili na Utambuzi wa Watu za mwaka 2014 ikiwemo Kanuni ya 7(3) (a) ambayo imeainisha taarifa zilizopo katika uso wa Kitambulisho cha Taifa zinazohusisha tarehe ya ukomo wa muda wa matumizi ya Kitambulisho cha Taifa ili kuondoa ukomo wa matumizi Marekebisho hayo yalitangazwa rasmi katika Tangazo la Serikali (GN) Na. 96 la tarehe 17 Februari, 2023,” amefafanua Naibu Waziri.
Ameongeza kuwa marekebisho hayo hayatahusu muda wa matumizi ya Vitambulisho vya Taifa kwa Wageni Wakaazi (Legal Residents) na Wakimbizi.