SERIKALI imetoa ufafanuzi juu ya kusimama kwa ndege za Shirika la Ndege nchini (ATCL), aina ya Airbus a220-300 na kusema zimepata hitilafu ya kiufundi na kuongeza kuwa serikali inaendelea na mawasiliano na watengenezaji wa ndege hizo, ili ziweze kuendelea na kazi.
Ufafanuzi huo umetolewa leo Januari 15 na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa wakati akizungumza na waandishi wa habari ikiwa ni muendelezo wake wa utoaji taarifa kwa umma na kuwahakikishia Watanzania kuwa zitakapokuwa sawa basi zitaendelea na safari zake.
“Ni mambo ya kawaida kimawasiliano na imetokea kwenye nchi nyingi tuu na ndege karibu duniani kote zimepata hiyo changamoto na kwa utaratibu wa usafiri wa anga, mtengenezaji anapobaini changamoto unasitisha safari, ili muweze kufanyia kazi hizo changamoto,” amesema.
Hata ndege zingine za Boeing kwenye nchi zingine pia zimepata hizo changamoto, lakini ndege zingine za shirika letu la ATCL zinaendelea kutoa huduma kama kawaida,” amefafanua Msigwa.