Serikali yatuliza wananchi mafuta ya kupikia

IKIWA ni takribani miezi sita sasa bado bei ya mafuta ya kupikia imeendelea kuwa mwiba, serikali imewatoa wasiwasi wananchi kwamba tatizo hilo linaelekea ukingoni baada ya wakulima kuvuna alizeti kwa wingi.

Kwa takribani miezi sita, bei ya bidhaa hizo imekuwa ikipaa kuliko kawaida katika mikoa mbalimbali nchini.

Akizungumzia suala hilo, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe alisema hali ya upatikanaji wa bidhaa hiyo kwa sasa inaridhisha baada ya wakulima kuvuna alizeti kwa wingi.

“Changamoto tuliyoiona sasa hivi, viwanda vingi baada ya muda si mrefu miezi miwili au mitatu vilikosa malighafi ambayo ni alizeti inayotumika kuchakata mafuta ya kula,” alisema.

Alieleza kuwa hamasa kubwa inayotumika na serikali ni kuhamasisha wakulima kulima mazao yanayotumika kuzalisha mafuta ya kula hasa alizeti.

Alisema hata Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, hivi karibuni akiwa Singida alitumia fursa hiyo kuhamasisha wakulima kuzalisha zao hilo la alizeti kwa wingi, ili kuzalisha mafuta ya kupikia ya kutosha nchini.

Katika uchunguzi uliofanywa na HabariLEO, pamoja na kauli hiyo, bado bei ya mafuta iko juu wakati mafuta kutoka nje gharama yake ikipungua kidogo.

Mmoja wa wafanyabiashara anayeuza duka eneo la Ubungo, Khalfan Mmanga alieleza lita tano ya Korie imefikia Sh 23,000 na mafuta ya Sundrop bei yake iko juu sana inafikia 35,000 hadi 36,000.

Alisema lita tatu ya mafuta hayo inauzwa Sh 20,000 kutoka 13,000 na lita moja iliyokuwa ikiuzwa Sh 5,500 sasa inauzwa Sh 8,000 mpaka 9,000. “Mafuta haya (Sundrop) yalipotea kabisa kipindi cha nyuma lakini baada ya kurejea sasa hayashikiki bei ni ya juu tunachukua tu.”

Mmoja wa mamalishe eneo la Tazara, Felista Peterson alisema bei ya mafuta imeathiri sana biashara yake hali iliyomlazimu kutumia kiasi kidogo sana cha mafuta na kusababisha malalamiko kwa wateja wake.

“Kwa kweli tunaumia, nimelazimika kuacha kupika baadhi ya vyakula vinavyotumia mafuta sana ili kupunguza gharama maana ukipandisha bei wateja nao hawanunui,” alieleza na kuongeza kuwa alikuwa akipika bagia lakini sasa anapika chapati.

Habari Zifananazo

Back to top button