KAMPUNI ya mtandao wa simu ya Airtel Tanzania imeingia katika ushirikiano wa kimkakati na Zanzibar Cable Television (ZCTV), ili kuwarahisishia wateja wao kufanya malipo ya huduma za ZCTV kupitia huduma za fedha ‘Airtel Money’.
Ushirikiano huo ni hatua muhimu katika kuunga mkono ajenda ya serikali ya kueneza uchumi shirikishi, na utoaji wa huduma za kifedha haraka na salama. Hii inadhirisha zaidi dhamira ya Airtel kukamilisha sera ya uchumi jumuishi kupitia huduma ya fedha kidijitali.
Akitambulisha ushirikiano huo, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Dk Khalid Mohamed alisema, “Ninawapongeza sana Airtel Tanzania pamoja na ZCTV kwa kuingia kwenye ushirikiano huu ambao pia unalenga kukuza uchumi wetu,”
“Ni furaha kubwa kuona taasisi binafsi zinakaa na kutengeneza ushirikiano ambao mbali na kuendelea kukuza bishara zao, pia inazidi kuongeza ajira, jambo ambalo serikali inaunga mkono,”. Aliongeza.
Mkurugenzi wa Huduma za Airtel Money Andrew Rugamba, aligusia faida watakayoipata pande zote za ushirikiano, akisema, “Airtel Money inalenga kutoa huduma zinazokidhi mahitaji yanayoendana na zama hizi za kidijitali kwa wateja wote,”
Alisema ushirikiano huu unawezesha wateja wa ZCTV kufanya malipo yao wakiwa popote kwa kutumia Airtel Money na kwamba lengo lao ni kurahisisha miamala ya kila siku, kuboresha uzoefu wa wateja wao na kuwawezesha watumiaji wa simu za mkononi kuzitumia kwa shughuli nyingi zaidi.
Rugamba alisema ushirikiano huu unatarajiwa kuleta faida kubwa kwa wateja wa pande zote mbili, sio tu kwa kurahisisha usimamizi malipo ya ZCTV kupitia Airtel Money bali pia kwa kuboresha vifurushi, kutatua hitilafu, na kupata maudhui ya moja kwa moja.
Mkurugenzi Mtendaji wa ZCTV, Hafidhi Kassim, alisifu uanzishwaji wa njia mpya ya malipo kwa ZCTV kupitia Airtel Money ambayo itawezesha upatikanaji rahisi wa huduma za ZCTV kuliko hapo awali.
“ZCTV imeazimia kuhakikisha kwamba wateja wetu wote wanafurahia kikamilifu huduma zetu, na tunaendelea kutafuta njia za kuboresha mipango ya kibiashara ili kutoa huduma bora kwa wateja wetu,” aliongeza.