Serikali yaungwa mkono tozo

Mfanyabiashara maarufu nchini, Azim Dewji

WAFANYABIASHARA, wachambuzi wa masuala ya uchumi na wanasiasa wamepongeza serikali kwa kuweka mfumo wa tozo ili kutekeleza miradi ya maendeleo.

Wamesema hayo jana katika mjadala wa kitaifa kuhusu tozo uliofanyika kwa njia ya Zoom ulioratibiwa na Taasisi ya Watch Tanzania.

Mfanyabiashara maarufu nchini, Azim Dewji aliipongeza serikali kwa kuwa sikivu na kupunguza tozo ambazo hazikuwaathiri wananchi wa kawaida, bali hata wafanyabiashara wakubwa hususani katika eneo la ushindani duniani.

Advertisement

“Kuna mapato mengi yanayoweza kukatwa kodi, Watanzania wenzangu tuwe tunaangalia serikali inafanya makubwa, Rais Samia haikuwa lazima kutoa shilingi bilioni 100 kama ruzuku ya mafuta angeamua tu kuacha na kusema bei ya mafuta imepanda duniani,” alisema Azim.

Alisema wapo mengi yanayotekelezwa na serikali kupitia tozo hizo kama vile kulipia ada shuleni ambako kwa sasa wanafunzi kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha sita wanasoma bila malipo.

“Sasa unapoondoa ada hizi lazima ufanye utaratibu wa kufidia bila kunyonya mwananchi na bahati nzuri serikali imefanya kwa uwazi kabisa kuhusu jambo hili kwamba itaweka tozo hizi,” aliongeza mfanyabiashara huyo.

Alitaja maeneo mengine ukiacha tozo ya miamala ya kielektroniki kuwa ni tozo ya reli wasafirishaji wanachangia moja kwa moja kutengeneza reli na tozo ya mafuta, ambayo mtu anapoendesha gari kila kilometa anayotembea anachangia Mfuko wa Barabara.

Pia aliitaja tozo ya kununua umeme kuwa tozo ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kupeleka umeme vijijini.

“Tozo kwa kweli inasaidia ingawa wachache ndio wanaoelewa. Jambo la msingi ni kwa Watanzania wote kusaidia serikali katika hili,” alisema Azim.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dk Abdallah Juma Sadallah (Mabodi) alisema tozo hizo zimekuja kutokana na hali ngumu ambayo nchi imepitia.

Alisema msimamo wa CCM ambayo ndiyo inayosimamia serikali ni kushusha tozo na kupunguza makali ya maisha kwa wananchi.

Aidha, alisema pamoja na hilo lililotokea ana imani na uhakika kuwa hadi mwaka 2025, Ilani ya Uchaguzi ya CCM itakuwa imetekelezwa ipasavyo na kwamba suala hilo la tozo haliwezi kukwamisha hilo.

“Msimamo wa chama ni kwamba saa zote tunakuwa karibu na wananchi, tunakwenda kwa wananchi na tunaondoa kadhia zote. Tunavaa nguo zile ambazo mwananchi anavaa, tunaangalia hali ilivyo kama tozo iongezwe au ipunguzwe. Ila ni vyema Watanzania wakaanza kujifunza kulipa kodi kwa hiari,” alisema.

Alisema chama hicho kiko macho na hakitapenda serikali yake iende kinyume na maagizo yake.

Kamishna Msaidizi wa Sera na Mapato katika Wizara ya Fedha na Mipango, William Mhoja akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba, alielezea namna serikali ilivyochukua hatua kupunguza maeneo matano ya tozo baada ya kuyafanyia tathmini.

Hata hivyo, aliweka bayana kuwa haiwezekani kufuta kabisa tozo hizo kwa sababu tayari kulikuwa na bajeti ambayo chanzo chake ni tozo hizo na ilishakadiriwa kuwa ni Sh bilioni 500 baada ya kupanua wigo na kujumuisha benki na huduma za simu.

“Kulikuwa na alternative (mbadala) kama mtu hatozwi kwenye simu anakimbilia kwenye benki…sasa katika kutanua wigo imeleta shida hii ambayo pia imeeleweka vibaya na kuonekana kama tumeingilia maeneo mengine lakini hatua ilikuwa ni kuongeza wigo,” alisema Mhoja.

Kuhusu kutafuta vyanzo mbadala vya mapato, alisema serikali imekuwa ikifanya tafiti na kuchukua maoni kutoka kwa wataalamu kila mwaka kuangalia maeneo yanayoweza kuingizia mapato.

Alikiri kuwa vyanzo vikuu vinavyoingizia serikali mapato mengi bado ni vilevile vya zamani ambavyo ni Kodi ya mapato, Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), kodi za kimataifa za kuingiza bidhaa na ushuru wa bidhaa.

Mtafiti wa Taaluma za Maendeleo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Hezron Makundi alisema fedha za tozo hizo ni muhimu kutokana na kugusa miradi inayogusa moja kwa moja wananchi kama vile miradi ya umwagiliaji, kutoa ada kwa shule za sekondari na shule za msingi, huduma za afya hadi vituo vya polisi.

Alisema wananchi wamekuwa wakisukuma serikali wakitaka maendeleo, lakini kuna baadhi ya mambo hayako chini ya uwezo wa serikali kama vile vita ya Ukraine na Covid-19 na hivyo kuamua kuja na njia mbadala za kutekeleza miradi hiyo.

 

 

 

 

/* */