Serikali yawahakikishia usalama wawekezaji Geita

GEITA: SERIKALI imetoa uhakika wa amani, ulinzi na usalama kwa wawekezaji wote ambao tayari wanafanya shughuli zao na wale wenye dhamira ya kufanya uwekezaji katika mkoa wa Geita.

Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani Geita imetoa kauli hiyo mara baada ya kufanya ziara ya kutembelea miradi mbalimbali ya umma na serikali wilayani Chato mkoani humo.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, Safia Jongo amesema jeshi la polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vimejizatiti kuhakikisha hakuna tishio la usalama kwa wawekezaji.

Kamanda Jongo alisema miongoni mwa fursa kubwa za uwekezaji mkoani humo ni upande wa sekta ya madini ambapo vijana wanapaswa kuitumia kujipatia kipato na kuepuka kufanya uharifu.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Mohamed Gombati amesema serikali inaunga mkono wawekezaji binafsi kwani wana mchango mkubwa katika kuchangia kukuza pato la taifa na mtu mmoja moja.

Gombati amesema serikali imeweka mazingira rafiki ya uwekezaji kwenye sekta zote ikiwemo madini, kilimo na mifugo ambapo taasisi zote zimejizatiti kuwapa ushirikiano wawekezaji.

Mkuu wa mkoa wa Geita, Martine Shigela amesema katika kufanikisha uwekezaji thabiti kwenye sekta ya madini serikali imenunua mitambo ya utafiti madini ili kuwezesha uchimbaji wenye tija.

Awali Mkurugenzi wa Tampmed Mining LTD, Ramadani Tampela alisema kampuni hiyo inatarajia kufanya uwekezaji wa zaidi ya sh bilioni 2 katika kiwanda cha uchenjuaji na usafishaji wa dhahabu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button