Serikali yaweka rekodi usajili miradi

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema katika kipindi cha mwaka 2021 hadi Januari, mwaka huu serikali imesajili miradi ya uwekezaji 537 yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 7,222.

Majaliwa alisema hayo Dar es Salaam jana alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa kituo cha biashara cha Afrika Mashariki kinachojengwa na kampuni ya East Africa Commercial and Logistics Center kwenye eneo la Ubungo.

Alisema hatua hiyo imetokana na kuboreshwa kwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na kuimarisha kituo cha huduma za mahala pamoja. Majaliwa alisema usajili wa miradi hiyo unatarajia kutoa ajira takribani 92,770.

“Kiwango hiki ni kikubwa kuwahi kuandikishwa katika kipindi chochote tangu nchi yetu ilipopata uhuru mwaka 1961,” alisema.

Majaliwa alisema serikali kupitia Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Mauzo ya Nje (EPZA) imesajili miradi 38 yenye thamani ya dola za Marekani milioni 139.70 na mauzo nje yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 191.04.

“Miradi hiyo ni mahususi katika sekta zinazozalisha bidhaa zitokanazo na kilimo, bidhaa za viwandani, bidhaa za mifugo, bidhaa za kemikali, bidhaa za madini na bidhaa za misitu,” alisema.

Majaliwa alisema kuna mazingira mazuri ya uwekezaji nchini hivyo ametoa mwito kwa wawekezaji kuja kuwekeza nchini kwani ni sehemu sahihi ya uwekezaji na kuleta mitaji yao.

Alisema mradi wa kituo cha biashara cha Afrika Mashariki utakuwa na maduka zaidi ya 2,000 yenye ukubwa tofauti hivyo kitapanua fursa ya Watanzania wengi kufanya biashara.

Majaliwa alisema kituo hicho kitatoa fursa kwa wamachinga kufanya biashara katika eneo la nje.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Angellah Kairuki alisema mradi huo una thamani ya dola za Marekani milioni 81.827.

Kairuki alisema mradi huo utaifungua Tanzania kibiashara na kukuza uchumi kutokana na biashara zitakazokuwa zikifanyika na kukuza uhusiano wa kimataifa kwa kuwa na mwingiliano wa wafanyabiashara.

Alisema kituo kitatoa ajira za moja kwa moja zaidi ya 15,000 na kuhamasisha  maendeleo ya sekta mbalimbali ambazo pia zitazalisha ajira zisizo za moja kwa moja 50,000 hivyo kuongeza mapato na kuboresha hali ya maisha kwa wananchi wa Tanzania.

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya East Africa Commercial and Logistics Center (EACLC), Dk Cathy Wang alisema mradi huo ukikamilika mapato ya jumla kwa mwaka yatafika zaidi ya dola za Marekani milioni 500.

Mradi huo utakuwa na maduka 2,060 yenye ukubwa wa jumla ya meta za mraba 75,000 na eneo hilo litakuwa na huduma za kibiashara zikiwemo benki na huduma za ufungishaji na usafirishaji.

 

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x