Serikali yazibana halmashauri tozo, ushuru wa mazao

Waziri Innocent Bashungwa

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa ameagiza halmashauri zote nchini kuhakikisha wanatekeleza mwongozo wa serikali wa kutotoza ushuru kwa wakulima wanaosafirisha mazao yao chini ya tani moja.

Bashungwa alisema hayo Alhamis jijini hapa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa mwongozo huo.

Alisema katika kuweka mazingira rafiki na wezeshi kwa wakulima, serikali ilitoa maelekezo ya kuhakikisha wakulima hawatozwi tozo wanaposafirisha mazao yao.

Advertisement

“Mpaka sasa bado maagizo ya serikali ya kutotoza ushuru wakulima wanaposafirisha mazao yao chini ya tani moja hayajabadilika. Bado maelekezo ya serikali ni kuhakikisha wakulima wanapovuna na kupeleka mavuno ya mazao kwenye magulio na masoko kama ni chini ya tani moja wasitozwe ushuru wowote,” alisema.

Bashungwa alimwelekeza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Tamisemi, Profesa Riziki Shemdoe kuhakikisha mwongozo huo unazingatiwa na wakurugenzi wote nchini. Aliwaelekeza pia wakuu wa mikoa na wilaya kusimamia mwongozo huo katika maeneo yao.

“Nitumie nafasi hii kuwaelekeza wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya katika maeneo yao kusimamia jambo hili ili lisifanyike kiholela. Kwa maeneo mengine wanatoza na maeneo mengine hawatozwi, kwa hiyo kunakuwa na mkanganyiko upande wa wakulima lipi ni lipi,” alisema.

Katika kutekeleza agizo hilo la serikali, Ofisi ya Rais-Tamisemi ilitoa mwongozo kwenye halmashauri zote namna ya kulitekeleza.

“Kwa hiyo ninakumbushia wakurugenzi waendelee kuzingatia mwongozo huo na wakuu wa mikoa na wilaya simamieni jambo hili kwani pamoja na jitihada kubwa ya kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya kumsaidia mkulima, Mheshimiwa Rais (Samia Suluhu Hassan) wetu anataka kumsaidia mkulima aweze kukua na kupambana na umasikini kupitia jasho lake la kilimo.”