SERIKALI imezindua mfumo kusajili kidijiti Watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora).
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax alisema mfumo una faida nyingi kwani unaweka taarifa za diaspora mahali walipo, taaluma zao, kazi wafanyazo na ujuzi wao.
Dk Tax alisema Dar es Salaam jana kuwa awali diaspora wa Kitanzania walikuwa wanapaswa kwenda kujisajili katika ofisi za ubalozi kwenye nchi alipo hivyo walitumia gharama kubwa na muda.
“Pamoja na umuhimu wa taarifa za diaspora kiuchumi na kijamii, taarifa sahihi husaidia kuwafikia diaspora kwa haraka na urahisi wakati wa majanga, mfano wakati Ukraine na Sudan zilipokumbwa na machafuko.
“Taarifa za Diaspora wetu ziliwezesha kuwatambua kwa haraka na kuwezesha kuwaondoa na kutoa misaada ya kibinadamu katika nchi hizo kwa haraka,” alisema Dk Tax.
Alisema kupitia mfumo huo wa kidijiti taarifa za diaspora zitakuwa salama kwa sababu sheria zaidi ya nne zinazolinda haki ya taarifa binafsi na haki ya kupata taarifa na nyingine zimezingatiwa.
Alisema mchango wa diaspora wa Tanzania katika nchi yao, Dk Tax unajionesha kwenye takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwamba katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2021 walituma fedha nchini zaidi ya Dola za Marekani milioni 569.3.
Aidha, kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka 2022, jumla ya fedha zote zilizotumwa na Diaspora nchini Tanzania kupitia vyanzo rasmi (miamala ya kampuni za simu na benki) ni Dola za Marekani bilioni 1.1 ambazo ni sawa na Sh trilioni 2.6 za Tanzania.
Dk Tax alisema mwaka 2022, uwekezaji uliofanywa na diaspora wenye asili ya Tanzania kwa ununuzi wa nyumba na viwanjani nchini ulifikia Sh bilioni 4.4 uwekezaji ambao ni nyongeza maradufu kutoka shilingi bilioni 2.3 walizowekeza diaspora katika nyumba na viwanja mwaka 2021.
“Takwimu kutoka Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja (UTT-AMIS), zinaonesha kuwa, katika kipindi cha mwezi Januari hadi Desemba 2022, diaspora wenye asili ya Tanzania waliwekeza katika skimu mbalimbali za UTT- AMIS kwa uwekezaji wenye thamani ya Sh bilioni 2.5,” alisema Dk Tax.
Alisema mfumo huo utaendelea kuimarisha uchumi wa nchi kwa kuweka taarifa za fursa lakini pia kujua utaalamu wa diaspora hao na kuwatumia na kusema usajili ni endelevu hivyo diaspora wote wajisajili.
Kwa mujibu wa takwimu kutoka Dawati ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, hadi sasa idadi ya diaspora wa Kitanzania nje waliojiandikisha ni zaidi ya milioni 1.5.