Serikali yazuia uuzaji viwanja kiholela

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angelina Mabula amepiga marufuku watu na kampuni wanaouza viwanja kiholela kwa viwango ambavyo havizingatii sheria ya mipango miji.

Akizungumza katika mkutano wa wadau wa sekta ya miliki Tanzania jana Dar es Salaam, Dk Mabula alisema kumetokea wimbi kubwa la uuzaji holela wa ardhi hasa viwanja ambavyo havijapimwa au kupangwa na wizara.

“Makampuni haya yananunua eneo na kuuza bila mpangilio, kampuni hizo tumeshazibaini na tutazichukulia hatua. Makampuni hayo yamekuwa yakinunua maeneo na kukata viwanja vidogo vidogo vya mita 300 jina maarufu 20 kwa 20, tutawachukulia hatua washiriki kwa sheria ya mipango miji na kufuata sheria,” alisema Dk Mabula.

Alisema wamekuwa wakipokea maombi kutoka kwa wananchi ya kutaka kupimiwa maeneo yao ambayo wanadai kuuziwa na baadhi ya kampuni yakiwa hayajapangwa wala kupimwa.

“Maeneo hayo barabara hazifiki upana wa mita nne na baada ya kuwauzia wananchi wanawaelekeza kufika wizarani kwa ajili ya kupimiwa, wakati huo wameshauza na kuleta migogoro ya matumizi,” alifafanua.

Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mipangomiji Namba 8 ya Mwaka 2007 Sura 355, Kifungu Namba 77 (1) (b), (i), Kanuni za viwango vya upangaji wa maeneo kwa mujibu wa Gazeti la Serikali la Machi 9, 2018, ukubwa wa maeneo kwa matumizi mbalimbali umeainishwa.

Alisema viwanja vya matumizi mbalimbali vinatakiwa kuwa na ujazo wa aina mbalimbali kama ujazo wa juu, ujazo wa kati na ujazo wa chini, na vinatakiwa kuwa na mapana na marefu yenye uwiano wa 1:2 mpaka 1:2.5.

“Kwa mfano, kiwanja chenye ukubwa wa mita za mraba 400 kinapaswa kuwa katika uwiano wa upana wa mita 16 na urefu wa mita 25, uwiano wa 1:1 yaani 20 kwa 20 haukubaliki kitaalamu na hakuna kiwanja chenye upana na urefu ulio sawa,” alisema Dk Mabula.

Alisema serikali inafanya marekebisho kwa kupitia sheria na kuandaa miswada kwa ajili ya kusimamia miliki.

“Tunahitaji kuwa na sera nzuri ambayo itasimamia milki na hadi sasa tumeshuhudia matokeo makubwa kama kuongeza idadi ya maeneo ya miliki, majengo yanaendelea katika miji, taasisi za nje zinashiriki katika uwekezaji wa nyumba, kuongeza katika taasisi ya fedha sasa kuna mabenki 33 yanatoa mikopo ya ujenzi,” alisema.

Aliziasa benki kutafuta mbinu ya changamoto ya riba kubwa ili wananchi wengi wamudu na waongeze wigo wa utoaji mikopo nafuu ya kujenga nyumba.

Alizitaka halmashauri zitenge maeneo ya kusubiri wawekezaji na si kuanza kuhangaika mwekezaji anapojitokeza ili kuongeza kasi ya wawekezaji na kuondoa usumbufu.

Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Allen Kijazi alisema takwimu za mataifa zinaonesha kuwa sekta ya miliki inachangia kiasi kikubwa kukuza mapato.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button