SERIKALI imesema ipo katika maandalizi ya kupanga bei linganishi ya mafuta ya dizeli, petroli na taa nchini ili kuondoa tofauti ya bei wakati wa ununuzi kati ya mkoa mmoja na mwingine.
Jambo hilo litasaidia wananchi waishio mikoa ya pembezoni kupata bidhaa hizo kwa bei nafuu.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, Januari 30, 2024 jijini Dodoma katika semina ya kuwajengea uwezo wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Sheria ndogo kuhusu majukumu, mafanikio na changamoto za EWURA.
“Serikali kupitia Wizara ya Nishati inaendelea na mikakati ya kupanga bei linganifu ya Mafuta ya Petroli, Dizeli na Taa kwa ajili ya kuondoa utofauti uliopo kati ya mkoa mmoja hadi mwingine wakati wa ununuzi wa Mafuta,” amesema Kapinga.
Kapinga amefafanua kuwa taratibu za kupanga bei linganishi ya mafuta katika Bandari ya Dar es salaam, Mtwara na Tanga zimekamilika na zitaanza kutumika mwezi Machi mwaka huu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Sheria ndogo, Dk Jasson Rweikiza ameipongeza Serikali kwa hatua hiyo na kusisitiza kuwa jambo hili litaleta nafuu kwa wananchi waishio katika mikoa ya pembezoni mwa nchi kama Kagera, Kigoma na Mtwara.
Semina hiyo imehudhuriwa na Watendaji mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).