Serikali za Afrika ziunge mkono mkakati wa AGRA kubadili kilimo

TAASISI ya Mapinduzi ya Kijani barani Afrika (AGRA) imezindua mkakati mpya wa miaka 5 unaolenga kuanzisha njia mpya ya kufanya kilimo katika bara hilo kuwa cha kisasa; lakini pia kusaidia serikali kuweka mazingira wezeshi kwa ushiriki wa sekta binafsi katika kuleta mabadiliko kwenye kilimo.

Mkakati huo ambao utekelezaji wake utagharimu dola milioni 550 ulizinduliwa kwenye kongamano la 12 la Mapinduzi ya Kijani Afrika (AGRF) Kigali Rwanda hivi karibuni.

Ukiangalia mkakati huo utabaini kwamba kuna mambo mengi ambayo yanahitaji ushirikiano wa dhati na  wa nguvu baina ya mataifa, serikali za mataifa hayo na sekta binafsi katika kufanikisha hilo.

Kutokana na ukweli huo tunaunga mkono hoja ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya AGRA, Hailemariam Desalegn aliyetaka serikali zote kushirikiana  kuhakikisha uwapo wa mifumo thabiti ya kilimo ili kujihakikishia usalama wa chakula na ubora wake.

Ni dhahiri kwamba mataifa ya Afrika kama yakifuata mkakati wa AGRA yatakuwa na uhakika na mifumo ya mbegu itakayochochea uzalishaji wa hali ya juu kutokana na kuwapo kwa mbegu bora na za uhakika zilizozalishwa kwa kuzingatia mazingira husika.

Mkakati huo ambao utawezesha  upatikanaji wa mbegu bora na za uhakika, pia unataja pembejeo ambazo kwa pamoja na mbegu  kunawezesha kilimo kuwa cha kisasa na chenye tija kubwa.

Tunaamini mkakati mpya wa AGRA utasaidia serikali nyingi  kuona njia  na fursa za kuleta mabadiliko ya mfumo wa chakula, kusaidia wakulima, na kuvutia uwekezaji hasa kutoka kwa vijana ambao ndio nguvu kazi inayoweza kuleta tafsiri mpya ya ajira mashambani kupitia kilimo biashara.

Katika vurugu na changamoto za  ajira katika nchi nyingi za Kiafrika, kwa kujikita katika kilimo cha kisasa na kukifanya kuwa kilimo endelevu, kutasaidia wakulima na jamii kujenga uendelevu wa biashara na maisha yao, kupitia ardhi, maji, na kilimo wanachohitaji.

Tunatoa shime kwa serikali za kiafrika kushirikiana na sekta binafsi kama ilivyoshauriwa na AGRA kuhakikisha kwamba mnyororo  wa kilimo bora unaendelezwa kwa kuhakikisha kwamba  kilimo kinalipa kwa kuwa na akiba ya chakula na pia kuna soko la uhakika la ziada yake huku vijana wakishawishika kujihusisha na kilimo biashara.

Tukizitaka serikali za kiafrika kuwa pamoja katika kuhakikisha kuna mabadiliko ya kilimo barani hapa na hivyo kuweka mataifa yao katika hali salama ya chakula, taasisi ya AGRA ambayo imekuwa msaada mkubwa wa mabadiliko ya kilimo, inafaa nayo kwa namna ya pekee kufuatilia mkakati wake.

Afrika inahitaji sio tu ushirikiano bali pia kuachana na siasa na kujikita katika ukweli wa kazi iliyopo mbele yetu ya kuhakikisha Bara hili halina shida ya chakula kwa kuhakikisha kuwa mifumo yake ya usalama wa chakula inafanyakazi inavyopaswa.

Na hili linapowezekana Afrika inakuwa ndio salama ya dunia katika chakula kwa miaka mingi ijayo.

 

Habari Zifananazo

Back to top button