SGR Uvinza-Musongati, funguo muhimu milango mipya ya uchumi

AGOSTI 16, 2025 serikali ya Tanzania na ya Burundi ziliweka jiwe la msingi kuashiria kuanza kwa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR kipande cha saba na nane kutoka Uvinza mkoani Kigoma hadi Musongati Burundi.

Uzinduzi wa mradi huo wa kihistoria kwa nchi hizo ulishuhudiwa na Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye na viongozi wengine wa nchi hiyo, kwa upande wa Tanzania Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.

Reli hiyo itakuwa na urefu wa kilometa 300, kilometa 240 za njia kuu na kilometa 60 za njia za kupishania na unatarajiwa kuwa na stesheni za kupakia abiria na mizigo.

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema kipande cha saba kutoka Uvinza-Malagarasi kitakuwa na urefu wa kilometa 190, kilometa 156 njia kuu na kilometa 34 njia za kupishania na cha nane kinachoanzia Malagarasi -Musongati kitakuwa na urefu kilometa 110, njia kuu kilometa 84 na kilometa 26 njia za kupisha kikiwa kimebuniwa mahususi kwa ajili ya kubeba mizigo mizito na abiria.

Kimsingi huu ni mradi mkubwa wa kwanza kutekeleza kwa ushirikiano wa nchi mbili katika ukanda wa Afrika Mashariki ni kielelezo cha ushirikiano mzuri baina ya nchi hizo.

SOMA: Ujenzi SGR Tanzania, Burundi ni ukombozi EAC

Waziri Mkuu Majaliwa anasema serikali ya Tanzania na ile ya Burundi zilikubaliana kujenga tawi la reli la Uvinza hadi Musongati kwa lengo la kuunganisha migodi inayopatikana katika maeneo hayo na Bandari ya Dar es Salaam inayosafirisha mizigo mingi katika ukanda huo.

Anasema, “Reli hii itarahisisha usafirishaji wa bidhaa ikiwemo madini ya nikeli, hivyo basi nikeli hii itasafirishwa na reli yetu tuliyonayo, hivyo inakwenda kuchochea mahusiano, biashara na kufungua fursa zaidi kiuchumi.”

Hatua hiyo ni moja ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayojielekeza katika kuifanya Tanzania ijiimarishe katika ushirikiano na nchi nyingine za Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) katika kuhakikisha sera za kikanda zinaakisi na kulinda maslahi ya kuichumi ya taifa na kuendeleza biashara na uwekezaji.

Majaliwa anasema mradi huu ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya dira na ajenda ya AU 2063 inayosisitiza kuunganisha nchi za Afrika kupitia miundombinu bora na ya kisasa ili kukuza mshikamano na ustawi wa maendeleo ya wananchi.

“Reli hii ni injini mpya ya uchumi wetu na ni Reli ya kwanza inayounganisha nchi na nchi kikanda,” anasema Majaliwa. Ujenzi wa reli hii utakuwa wa kipindi cha miaka mitano na mwaka mmoja wa matazamio. Mradi huo utagharimu Dola za Marekani bilioni 2.1 sawa na Sh trilioni 5.1 na unatarajiwa kuzalisha ajira za moja kwa moja 5,000.

Profesa Mbarawa anataja faida za reli hii pale itakapo kamilika na kuanza kutumika kuwa ni kupungua kwa gharama za usafirishaji mizigo kutoka Dar es Salaam hadi Bujumbura kwa asilimia 40. Anasema kwa sasa kusafirisha kasha moja kutoka Tanzania kwenda Burundi ni Dola za Marekani 3,800 (Sh milioni 9.9) lakini reli hii itapunguza na kufikia Dola 2,000 (Sh milioni 5.2) kwa kasha moja.

Aidha reli hiyo itawezesha usafirishaji wa mizigo mingi kwa wakati mmoja ikilinganishwa na ilivyo sasa na kupunguza muda uliokuwa unatumika kusafirisha mizigo. Kwa sasa sasa safari moja huchukua muda wa saa 96 takribani siku nne hadi tano lakini itakaposafirishwa na reli hii itachukua saa 20 pekee.

Profesa Mbarawa anasema kwa sasa lori moja lina uwezo wa kusafirisha tani 30 lakini reli hiyo ikianza usafirishaji
itasafirisha tani 3,800 kwa safari moja. Reli hiyo pia itatumia nishati ya umeme utakaozalishwa kwa kutumia
vyanzo vya asili na kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa ambayo ni ajenda ya nchi nyingi duniani.

Kadhalika reli hiyo itawezesha migodi ya nikeli iliyopo Musongati, Burundi kusafirisha madini yake hadi Bandari ya Dar es Salaam na mradi huo utaboresha maisha ya watu. Profesa Mbarawa anasema mradi huo utakapokamilika utatoa fursa kwa nchi za EAC kufanya biashara na kuimarisha utangamano wa kikanda na kuleta ustawi wa jamii.

Faida nyingine ni kuongeza ufanisi wa bandari ya Dar es Salaam kwa kuwa na uwezo wa kuzihudumia nchi zinazotumia bandari hiyo na kuimarisha ushoroba wa kati katika biashara za kikanda.

Reli hiyo pia inatarajiwa kukuza uchumi wa kikanda kwa kuunganisha masoko yaliyopo nchini na yale ya nchi za nje na kuimarisha upatikanaji wa huduma muhimu za usafirishaji katika maeneo hayo na itakuwa kichocheo cha maendeleo ya viwanda, kilimo, sekta ya madini na sekta nyingine za uzalishaji kwa kutoa huduma ya usafiri wa uhakika.

Kwa upande wake Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye, anasema utekelezaji wa mradi huo utatoa fursa mpya za kibiashara na kuimarisha mtangamano wa kikanda. “Reli hii itafungua fursa mpya za kibiashara, kuongeza ajira na kuimarisha mshikamano wa kikanda, ni hatua kubwa kuelekea mustakabali wa ustawi wa watu wetu,” anasema Ndayishimiye.

Naye Waziri Mkuu wa Burundi, Nestor Ntahontuye anasema reli hiyo italeta mageuzi makubwa katika sekta
ya usafirishaji na kufungua milango ya uwekezaji mpya nchini Burundi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button