SERIKALI imesema katika mwaka wa fedha 2023/2024 imetenga Sh bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya zitakazosaidia kuongeza madarasa katika shule za msingi, hivyo kuondokana na msongamano wa wanafunzi darasani.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI anayeshughulikia elimu, Deogratius Ndejembi, wakati akijibu swali la Mbunge wa Tarime Mjini, Mwita Michael aliyehoji mkakati wa serikali katika kuondoa tatizo la wanafunzi kusoma kwa zamu katika Halmashauri ya Mji Tarime.
Akijibu swali hilo bungeni jijini Dodoma kwa niaba ya Waziri wa TAMISEMI, Ndejembi amesema kuwa Halmashauri ya Mji wa Tarime imeshatenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ili kuondoa msongamano wa wanafunzi pamoja na kuondoa tatizo la wanafunzi kusoma kwa zamu.
“Baadhi ya maeneo tayari wananchi wameanza kujenga shule, mfano Kata ya Turwa, Chira-Kenyamyori,” amesema Ndejembi.