Sh Bil 1.6 kumaliza kero ya maji vijiji 3 Kilolo

WANANCHI katika Vijiji vitatu vya Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, wanatarajiwa kunufaika na mradi wa maji wa Masalali, Masege na Kihesa Mgagao ambao ujenzi wake unatarajiwa kuanza hivi karibuni ukigharimu zaidi ya Sh Bilioni 1.6.

Kukamilika kwa mradi huo kutanufaisha zaidi ya wananchi 5543 wa vijiji hivyo na kuwaondolea adha ya upatikanaji wa huduma hiyo katika maeneo yao.

Tarifa hiyo imetolewa katika hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mradi huo kati ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) na Mkandarasi Mponela Construction JV Dimotoklasa mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Peres Magiri aliyesisitiza uzalendo na uadilifu katika kuutekeleza.

Mkuu huyo wa wilaya amemsisitiza mkandarasi kukamilisha mradi huo kwa wakat,i huku akizingatia viwango vinavyoendana na thamani ya fedha zilizotolewa na serikali.

“Tatizo kubwa la wakandarasi wengi ni kutokuzingatia muda wa kukamilisha mradi, hivyo ninyi mmetuhakikishia mna uwezo na hii kazi tuna imani ndani ya miezi nane mradi utakamilika kama ilivyo katika mkataba, hivyo mfanye kwa ubora na kwa kuzingatia muda wa ukomo,” alisisitiza

Mbali na hayo Magiri alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka fedha za utekelezaji wa miradi ya maji, ambayo mpaka sasa imewezesha asilimia 74 ya wananchi wa wilaya hiyo kufikiwa na huduma hiyo.

Awali Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Iringa, Mhandisi Joyce Bahati alisema katika bajeti ya mwaka 2023/2024 wamepokea zaidi ya Sh Bilioni 10.4 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji ndani ya mkoa huo.

“Tuna jumla ya miradi 36 tunayoitekeleza katika mwaka huu wa fedha; miradi 22 ni mipya ukiwemo huu wa leo na miradi 14 ni ile iliyovuka mwaka. Upatikanaji wa maji kwasasa ni asilimia 74.57 hivyo hadi kufikia mwezi Desemba tutafika asilimia 87.7,” amesema Mhandisi Joyce.

Mhandisi Joyce ameongeza kwa kuwataka wananchi kuwa walinzi sehemu inapopita miundombinu hiyo ikiwa ni pamoja na kujiepusha kuharibu, kufanya shughuli za kibinadamu kama kukata miti hovyo na kulima karibu na vyanzo vya maji.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Mponela Construction JV Dimotoklasa, Dickson Mwaipopo amesema kuwa muda uliopangwa kutekeleza mradi huo unatosha kabisa huku akisema baadhi ya kazi zisizohitaji ujuzi mkubwa watawatumia mafundi wazawa waliopo maeneo ya jirani na ulipo Mradi.

Habari Zifananazo

Back to top button