DODOMA; SERIKALI imesema katika mwaka wa fedha wa 2023/24 imetenga bajeti ya shilingi billioni 10.312 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya stendi katika halmashauri nchini.
Pia serikali imesema itaendelea kujenga stendi za mabasi katika halmashauri kwa awamu kupitia programu mbalimbali kama TACTIC, TSCP na vyanzo vingine yakiwemo mapato ya ndani Halmashauri.
Kauli hiyo imetolewa bungeni na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Festo Dugange alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mwantum Zodo aliyetaka kujua serikali ina mpango gani wa kujenga stendi za mabasi katika Halmashauri za Mkoa wa Tanga.
“Serikali kupitia Mradi wa uboreshaji wa Majiji na Manispaa Tanzania (TSCP), imejenga stendi ya kisasa katika Jiji la Tanga na Halmashauri ya Mji Korogwe zilizogharimu takribani kiasi cha shilingi billioni 10.7, ujenzi wa stendi hizo umekamilika na zinatumika.
“Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha wa 2023/24 Serikali imetenga bajeti ya shilingi billioni 10.312 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya stendi katika halmashauri nchini.
“ Aidha, serikali itaendelea kujenga stendi za mabasi katika halmashauri kwa awamu kupitia programu mbalimbali kama; TACTIC, TSCP na vyanzo vingine yakiwemo mapato ya ndani Halmashauri,” amesema Naibu Waziri.