Sh Bil 131 zatumika miradi mbalimbali Wilaya Tanganyika

ZAIDI ya Sh Bilioni 131 zimekusanywa, kupokelewa na kutumika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo iliyopo Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025 katika wilaya hiyo kwa kipindi cha miaka miwili( Machi 2021- 2023 ) cha serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Ameyasema hayo katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Tanganyika kilichoketi Aprili 5, 2023.

DC Buswelu amesema fedha hizo shilingi 131,791,925,200.5 zimefanikisha kuifungua Tanganyika katika maeneo mbalimbali ikiwemo afya,  barabara, kilimo, elimu, maji, mawasiliano na uchukuzi, umeme vijijini, uwekezaji na sekta mbalimbali.

Katika sekta ya afya ndani ya miaka miwili, wilaya hiyo ilipokea zaidi ya Sh bilioni 4, ambazo zimetumika katika ujenzi wa miundombinu ya afya kama ujenzi wa jengo la wagonjwa mahututi na ujenzi wa wodi tatu katika Hospitali ya Wilaya ya Tanganyika, ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya, zahanati na nyumba za watumishi.

Amesema, katika sekta ya barabara Wilaya ya Tanganyika sasa imeunganishwa na mtandao wa barabara hali inayochochea uwekezaji, ikiwemo wananchi kujiingizia kipato kupitia usafiri na usafirishaji.

“Ujenzi wa barabara ya Vikonge – Luhafye yenye urefu wa Km 25 inayojengwa kwa fedha za kitanzania zaidi ya bilioni 35 mkandarasi yupo eneo la mradi na ujenzi unaendelea, barabara ya Kagwira – Ikola – Karema yenye urefu wa Km 120 ipo hatua ya awali ya upembuzi na kiasi cha shilingi bilioni 1.073 kimetolewa,” amesema.

Barabara nyingine zinazotengenezwa chini ya TANROADS ni ya Kibo – Mwese – Lugonesi, Kagwira – Karema na Mpanda – Uvinza huku Wakala wa Barabara za Mjini na vijijini TARURA akiongezewa bajeti kutoka Sh 641,150,000 mwaka wa fedha 2020/21 hadi kufikia Sh 4,157,455,928.18 kwa mwaka wa fedha 2022/23 sawa na ongezeko la asilimia 259.

Amesema sekta ya elimu imeimarika mara dufu baada ya kujengwa miundombinu ya kutosha, ambapo kupitia fedha za UVIKO-19 jumla ya vyumba vya madarasa 196 vimejengwa ( shule ya msingi  vyumba 127 na shule za Sekondari vyumba 69) na kupitia fedha za mapato ya ndani na hewa ukaa jumla ya vyumba 94 vimejengwa, ikiwemo kujenga shule mpya ya Majalila.

Pia chuo cha ufundi stadi (VETA) ujenzi wake unatarajia kuanza mwezi huu eneo la Kijiji cha Majalila.

Maeneo mengine aliyoyataja wilaya hiyo kupiga hatua ni sekta ya maji, ambapo  Sh 6,481,086,307.46 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji, ambapo miradi 15 itakayonufaisha vijiji 22 inajengwa na baadhi imeanza kutoa huduma.

Amesema sekta ya maliasili na utalii imezidi kuimarika ambapo kutokana na utunzaji na usimamizi mzuri wa maliasili na misitu, jumla ya vijiji 8 vya Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika vimenufaika na mradi wa hewa ukaa ambapo shilingi bilioni 6.57 zimepatikana ndani ya miaka miwili.

Fedha hizo zimetumika kujenga madarasa, zahanati, kuajiri walimu wa mikataba, kutoa vyakula kwa wanafunzi shuleni, kuajiri askari walinzi wa misitu na kukopesha vikundi vya wajasiriamali vijijini kupitia (COCOBA).

Habari Zifananazo

Back to top button