Sh Bil 19 kuboresha miundombinu ya maji Mtwara

SERIKALI imetoa kiasi cha sh bilioni 19 kwa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mtwara (MTUWASA), kwa ajili ya uboreshwaji wa mtandao wa miundombinu ya usambazaji maji mji wa Mtwara.

Waziri wa Maji Jumaa Aweso ametoa taarifa hizo, wakati akishuhudia utiaji saini mkataba wa utekelezaji wa mradi huo kati ya MTUWASA na mkandarasi, ambaye anatarajia kutekeleza mradi huo.

Akizungumza mara baada ya kushuhudia zoezi hilo, Aweso amewataka mamlaka ya maji mji wa Mtwara kuhakikisha wanasimamia mradi huo, ili utekelezwe kama ilivyopangwa na kuleta matokeo ya kuwanufaisha walengwa.

“Tusimamie mradi huu, moja ya changamoto ya miradi ya maji ni usimamizi ndugu zangu, hizi ni fedha zenu, bilioni kumi na tisa zimeletwa kwa ajili ya kuwanufaisha, hivyo lazima tusimamie kwa dhati na kuleta matokeo,” amesema.

Waziri amemtaka mkandarasi kuhakikisha anatekeleza na kukamilisha mradi huo ndani ya mwaka mmoja, huku akimtaka kushirikiana na viongozi wa mkoa, watendaji wabunge na madiwani, ili mradi utekelezwe na kukamilika ipasavyo na kuwanufaisha wananchi waliokusudiwa.

“Watu wanataka maji wewe (mkandarasi) kazi yako ni kuwapatia huduma ya maji, sio umepata kazi unaanza blabla ,tutakuja kugombana, umepata kazi fanya kazi,” amesema na kumtaka mkandarasi huyo kutoa ushirikiano kwa viongozi wa mkoa na watendaji pamoja na wawakilishi wa wananchi kuhusu utekelezaji wa mradi huo.

Aweso pia aliwaomba viongozi wa mkoa na wawakilishi kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa mradi huo na kutaka taarifa ya maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo.

Mkurungenzi Mtendaji wa MTUWASA, Mhandisi Rejea Ng’ondya, ameshukuru serikali kwa kutoa fedha hizo, huku akisema serikali imewapa upendeleo wa hali ya juu wana Mtwara.

Ng’ondya amesema miundombinu ya usambazaji maji mji wa Mtwara imechakaa  baada ya kutumika kwa muda mrefu bila kubadilishwa.

“Miundombinu ya usambazaji maji mji wa Mtwara ni ya muda mrefu sana, hivyo kuchangia uwepo wa changamoto katika usambazaji wa maji mjini Mtwara,” amesema na kuongeza kuwa fedha ambazo zimeletwa na serikali zinaenda kutatua changamoto hiyo na kuweza kusambaza maji kwa wananchi wengi zaidi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button