SERIKALI imesema kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo ilitoa mikopo ya Sh bilioni 47.042, ili kuwezesha uwekezaji katika viwanda vya uchakataji na uongezaji thamani wa mazao mbalimbali nchini.
Akiwasilisha bajeti ya makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Waziri wa wizara hiyo, Ashatu Kijaji amesema mikopo iliyotolewa imefanikisha uwekezaji katika viwanda vipya 5 na viwanda 9 vilivyokuwepo kupitia mikopo ya uendeshaji na ununuzi wa mashine za kisasa.
Akizungumza bungeni jijini Dodoma, Kijaji amesema mikopo iliyotolewa kwa viwanda vipya inajumuisha kiwanda kikubwa cha uzalishaji wa sukari kilichopo Bagamoyo ambacho kimeanza uzalishaji kwa kusaga tani 1,500 za miwa kwa siku na kiwanda cha kukoboa mpunga na utengenezaji wa chakula cha mifugo chenye uwezo wa kukoboa tani 192 za mpunga kwa siku.
Mikopo hiyo pia inajumuisha utengeneza wa tani 240 za chakula cha mifugo kwa siku kilichopo 36 Kahama, Kiwanda cha uzalishaji wa mafuta ya kupikia ya mawese kilichopo Kigoma chenye uwezo wa kuzalisha tani 1 ya mafuta ghafi kwa saa na lita 2,000 za mafuta yaliyosafishwa kwa siku. Kiwanda hiki kipo Kigoma.
Vile vile, viwanda viwili vya usindikaji wa maziwa vilivyopo Tanga na Kagera vyenye uwezo wa kusindika lita 120,000 na lita 10,000 za maziwa mtawalia; na kiwanda cha uzalishaji wa mchuzi wa zabibu kilichopo Dodoma chenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 3 za mchuzi kwa mwaka vilinufaika na mikopo.
Amesema jumla ya Sh bilioni 8.725 zilitolewa kusaidia viwanda vidogo vidogo vya uchakataji wa mazao ya alizeti, mawese, usagaji wa unga wa mahindi, ukoboaji wa mpunga vilivyopo katika maeneo mbalimbali nchini.