Sh bilioni 1.4 kukamilisha ujenzi Shule ya Barbro

DAR ES SALAAM: KIASI cha Sh bilioni 1.4 kinahitajika ili kukamilisha ujenzi wa jengo la Tehama la Shule ya sekondari ya Wasichana ya Barbro Johansen ya jijini Dar es Salaam.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Bodi ya shule hiyo Profesa Anna Tibaijuka akizungumza na vyombo vya habari jana baada ya uzinduzi wa ujenzi wa jengo hilo ulioambatana na na mahafali ya 18 ya kidato cha sita yaliyofanyika shuleni hapo Luguruni wilayani Ubungo.

“Tuna mshukuru Mungu kwa kiasi cha Sh 72 milioni zilizokusanywa leo, na kiasi cha Sh milioni 500 zilizoahidiwa na hivyo kuwaomba wadau wa elimu na wapenda mendeleo hususani sekta ya Tehama kutuunga mkono katika uchagiaji wa ujenzi wa jengo la Tehama na ununuzi wa vifaa vya Tehama” amesema Prof Tibaijuka

Aidha Profesa Tibaijuka amesema shule hiyo imekuwa msaada na kimbilio kwa wanafunzi wahitaji ambapo katika wanafunzi 120 waliohitimu kati yao wanafunzi 72 wamepatiwa ufadhili wa moja kwa moja na uongozi wa shule hiyo kwa maana elimu bila malipo.

SOMA: Mikopo kumaliza changamoto TAMONGSCO

Vilevile Prof Tibaijuka ameishukuru serikali ya Sweden ambayo imetoa mchango mkubwa katika ujenzi na uanzishwaji wa shule hiyo ambayo imekuwa kimbilio la wengi katika huduma ya elimu nchini.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Fedha wa Benki ya CRDB na aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, Fedrick Nshekanabo amesema benki yao ni mdau mkubwa wa elimu nchini na mshirika mkubwa shule ya Barbro na hivyo mafanikio ya Barbro nyuma yake kuna mchango mkubwa benki hiyo na wao watachangia Sh milioni 500.

“Tutaendelea kuchangia katika maendeleo ya elimu ikiwemo shule ya sekondari ya wasichana ya Barbro,ninaamini kituo hiki cha Tehama kwa namna nlivyoona mchoro wake kitakuwa kituo bora barani afrika na kwanza kiukubwa nchini Tanzania, hivyo nawasihi watanzania kuwekeza zaidi katika elimu na Tehama zaidi ili kujipatia maendeleo” amesema Nshekanabo

Aidha Nshekanabo ameipongeza menejiment, bodi na wanafunzi wa shule hiyo kwa jitihada zao katika kuhakikisha wanafunzi wanafanya vizuri na akiwasihi wahitimu kwenda kuwa raia wema na kujiendeleza zaidi kitaaluma hadi ngazi ya udaktari wa falsafa.

Mkuu wa shule hiyo, Jospina Leonidace amesema shule yao hufanya vizuri kitaaluma katika mitihani ya kikanda, kimkoa na kitaifa na hivyo kuwaomba wazazi kupeleka Watoto wao katika shule hiyo.

Habari Zifananazo

Back to top button